MARA ya tatu? Haiwezekani. Hiyo ni kauli
ya nahodha wa Simba, Jonas Mkude, akisema hawapo tayari kufungwa mara ya tatu
mfululizo na Yanga wakati timu hizo zinapokutana leo.
Yanga na Simba leo zinacheza mechi ya
Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku kukiwa na kumbukumbu
ya Simba kufungwa na Yanga mechi mbili zilizopita.
Mkude ambaye amekuwa nguzo muhimu kwenye
kiungo cha Simba, alisema mchezo wa leo ni muhimu zaidi kwao na wana lengo la
kushinda.
“Haitapendeza kuona tunapoteza mechi hii
dhidi ya Yanga kutokana na mambo mawili yaliyopo mbele yetu, kwanza tunataka
ubingwa, hivyo tumekubaliana kushinda kila mechi ikiwemo hii na Yanga.
“Pili, hatuwezi kukubali kufungwa mechi
ya tatu mfululizo na Yanga kwani msimu uliopita wametufunga mechi zote mbili,
hii inatuumiza na tumepanga kufuta vipigo hivyo,” alisema Mkude.
“Tumefanya maandalizi ya kutosha,
tutaingia uwanjani tukiwa na ari ya kupambana kutokana na matokeo ya mechi zetu
za nyuma na tuna morali ya kuwa kileleni, hivyo hatutaki kupoteza mechi.”
“Hakuna namna, lazima tushinde mchezo huu
ili kufikia malengo tuliyojiwekea, kama tukifungwa itakuwa aibu kwetu kufungwa
na Yanga mechi tatu mfululizo,” alisema Mkude.
Post a Comment