SOKA ni
mchezo wa furaha, amani na upendo. Pale unapogeuka uadui uwanjani ni jambo la
hatari kwa wachezaji. Straika wa kimataifa wa Stand United, Abasirim
Chidiebere, kamwe hatamsahau beki shupavu wa Azam FC, Aggrey Morris, kwa
kitendo alichomtenda kwa kumfanyia rafu mbaya ambayo imemfanya kuwa nje ya
uwanja kwa wiki sita.
Chidiebere
ambaye ni raia wa Nigeria, aliumizwa na Aggrey Oktoba 12 mwaka huu wakati wa
mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Stand United na Azam mchezo uliochezwa
Uwanja wa CCM Kambarage na kumalizika kwa ‘Wapiga debe’ hao wa Shinyanga
kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Straika huyo
anamtuhumu Aggrey kwa namna alivyomfanyia ukatili wa kumchezea rafu
iliyomsababishia kuvunjika taya na kuwekwa nyaya maalumu kuzuia meno yasitoke
huku akiendelea kula kwa kutumia mrija.
DIMBA
limefanya mazungumzo na straika huyo kujua mwendelezo wa afya yake baada ya
kukumbwa na ajali hiyo akielezea masikitiko yake kwa kufanyiwa kitendo hicho
alichokiita si cha kiungwana.
DIMBA: Pole
kwa majeraha uliyoyapata.
Chidiebere:
Asante kikubwa nashukuru bado navuta pumzi.
DIMBA: Unaweza
kuelezea tukio la kuumizwa lilikuwaje?
Chidiebere:
Naumia sana ninapofikiria tukio lile
kwani sikudhani mchezaji mkubwa mwenye heshima katika soka la Tanzania kama
Aggrey Morris angeweza kunifanyia kitu kama kile kwa makusudi wakati sina
ugomvi naye.
Ninachokumbuka
tulikuwa tunawania mpira kama ilivyo kawaida ya straika na beki lakini ghafla
nikashtukia napigwa kiwiko na kuanguka nikiwa nagalagala nikashangaa anainua
miguu na kunikanyaga kama njia ya kunikomesha. Baada ya hapo sikujua
kilichoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo kwenye chumba cha
wagonjwa nikipatiwa huduma ya kwanza na madaktari.
DIMBA:
Ilikuwaje baada ya hapo?
Chidiebere:
Nilipozinduka nakujiona nipo kwenye chumba nikagundua nilikuwa nimepoteza
fahamu kwani niliwaona madaktari pamoja na viongozi wakiwa pembeni yangu, baada
ya kufumbua macho nilisikia wakiambiwa watoke nje ili matibabu yaendelee,
kiukweli namshukuru Mungu kuendelea kuwa hai mpaka leo.
DIMBA: Kabla
ya Aggrey kukuchezea rafu ulishawahi kuwa na tatizo lolote ambalo linasababisha
kuzimia?
Chidiebere:
Hapana, katika maisha yangu sijawahi kuzimia, hii ni mara ya kwanza ndiyo maana
mara kwa mara namshukuru Mungu kwani sidhani kama nilitakiwa kuendelea kuvuta
pumzi kama si mapenzi yake.
DIMBA:
Alichokifanya Aggrey kwako ni mchezo au mlikuwa na ugomvi nje ya uwanja?
Chidiebere:
Katika vitu nisivyovipenda katika maisha yangu ni kukwazana na mtu na hata kama
kuna nililomkosea anapaswa kuniambia si kunifanyia jambo kama hili
lililohatarisha maisha yangu.
DIMBA: Kwa
maana hiyo unafikiri Aggrey alikusudia jambo baya kwako?
Chidiebere:
Ndiyo, tena naweza kusema alipanga kuniua ila Mungu hakuwa upande wake,
nashangaa kwanini hadi sasa hakuna jambo lolote la kisheria lililochukuliwa na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
DIMBA:
Unafikiri TFF walipaswa kufanya nini juu ya hili.
Chidiebere:
Michezo ya kibabe na rafu zisizo za michezo kwa Aggrey hazikuanza leo, nafikiri
unakumbuka yaliyomkuta Okwi, nakumbuka alifungiwa baadhi ya mechi lakini adhabu
hiyo haitoshi.
DIMBA:
Adhabu gani anastahili?
Chidiebere:
Kufungiwa maisha kwani kama ameweza kufanya kwa Okwi aliyepoteza fahamu akaja
kwangu nimepoteza fahamu na kunivunja taya ipo siku atakuja kufanya jambo
litakalosababisha mchezaji kupoteza
uhai.
DIMBA:
Unafikiri kwanini TFF wamekuwa kimya hadi sasa?
Chidiebere:
Kwa kuwa sichezi katika timu zenye faida kwao kwa maana Yanga na Simba
inakumbukwa yalipomkuta Okwi waliingilia kati na kutoa adhabu, mbona kwangu
wapo kimya, je, angekuwa mchezaji wa timu zao wangefanya kama ilivyo sasa.
DIMBA: Kwa
upande wa Azam na Aggrey tangu litokee jambo hilo wameshakujulia hali?
Chidiebere:
Walikuja kuniona kambini mara baada ya kurejea hospitali na viongozi wa Azam
waliahidi kunisaidia lakini hadi hivi sasa hakuna aliyenipigia simu hata
kunijulia hali zaidi ya mabosi zangu Stand United wanaogharamia huduma zote za
matibabu.
DIMBA:
Unatibiwa hospitali gani na kwa mujibu wa daktari utakuwa nje kwa muda gani?
Chidiebere:
Napata matibabu katika Hospitali ya Faha dental Clinic na nitakuwa nje ya
uwanja kwa wiki sita huku kila siku nikitakiwa kuripoti kwa ajili ya uchunguzi.
DIMBA:
Matabibu wanasemaje, taya zikikaa sawa unaweza kurejea uwanjani?
Chidiebere:
Walichoniambia zimevunjika vibaya hivyo jibu kamili la kucheza au la
litajulikana baada ya muda huo.
DIMBA:
Kulingana na tatizo hilo jambo gani unadhani limevurugika?
Chidiebere:
Kwanza mfumo wangu wa maisha, nilikuwa naongea lakini hivi sasa siwezi,
nilikuwa nakula mwenyewe lakini tatizo hili natumia mirija, kikubwa zaidi
nafikiria itakuwaje kama suala hili halitapona si ndio nitakuwa nimepata
ulemavu, itakuwaje maisha yangu kwani mpira ndiyo kazi inayofanya familia yangu
iweze kuishi vizuri.
DIMBA: Nini
unachoweza kumwambia Aggrey kwa hivi sasa?
Chidiebere:
Mpira ni mchezo wa furaha si vita, hata kama wachezaji watakuwa na ugomvi basi
uishe nje ya uwanja tunapoingia uwanjani
tupo kazini.
Alifanya
haya kwa Okwi, kwangu na hivi karibuni amefanya hivyo kwa Simon Msuva na Obrey
Chirwa katika mechi yao na Yanga japo hao wawili hawajapata madhara kama sisi.
Siku zote
beki bora anaweza kuwa ni yule anayezuia zaidi au kuisaidia timu yake
kutofungwa kwa kuokoa au kuvuruga mipango ya wapinzani lakini si kwa sifa
nyingi za kuwaumiza wengine.
MAKALA HII IPO
KWENYE GAZETI LA DIMBA LA LEO
Post a Comment