LAUDIT Mavugo amepewa mechi nane tu kuhakikisha
anaongeza ubora wake wa kushirikiana vizuri na Ibrahim Ajibu na washambuliaji
wengine wa Simba.
Licha ya timu hiyo kucheza mechi saba mpaka sasa
bila ya kufungwa na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara lakini benchi
la ufundi la timu hiyo chini ya Mcameroon, Joseph Omog limeeleza kinagaubaga
kuwa baada ya mechi hizo wanaamini safu yao ya ushambuliaji itatisha zaidi.
Kocha msaidizi wa Wekundu hao, Mganda, Jackson
Mayanja ameliambia Championi Jumatatu kuwa kila mchezaji sasa ameingia kwenye
mfumo na kutengeneza maelewano mazuri isipokuwa wachezaji watatu; Mavugo,
Muivorycoast, Fredric Blagnon na Ajibu.
“Kila kitu kimekaa sawa kwenye timu isipokuwa
hawa watatu, yaani kama ‘combination’ yao ingeelewana mapema basi kazi ya msimu
huu ingekuwa rahisi. Kinachokwamisha ni kuelewana kwa safu ya ushambuliaji kati
ya Ajibu, Mavugo na Blagnon.
“Si lazima wote watatu waanze pamoja lakini
tunachokilenga hapa kwamba wakianza wawili kati yao wafanye vizuri na akitoka
mwingine akiingia mwingine iwe hivyohivyo, hili linamlenga mpaka Ame Ali siyo
kina Mavugo pekee.
“Utendaji wao unahitaji kuboreshwa zaidi na hili
ndiyo tunalolifanyia kila siku kwa sasa, tunataka mpaka mwisho wa mzunguko wa
kwanza uliobakisha mechi nane hili suala liwe limekwisha, tukianza mzunguko wa
pili, tuwe fiti kila mahali, tunajaribu kuwaelekeza lakini na wao pia lazima
wafanye juhudi,” alisema Mayanja.
Kuhusiana na utendaji kazi wa Shiza Kichuya
kikosini hapo, Mayanja alisema: “Kichuya anafanya vizuri, anafunga na
anapambana, yeye amezoea mazingira mapema kwa kuwa yupo kwenye hii ligi tangu
msimu uliopita lakini Mavugo na Blagnon ni wageni na wanahitaji kuongeza bidii
kuzoea mazingira mapema sana.
“Bado tunahitaji mabao mengi ya kufunga, kwa hiyo
ukichanganya haya ya Kichuya na yatakayopatikana kutoka kwa kina Mavugo,
tutakuwa mbali.”
Simba imefunga mabao 13, katika hayo safu ya kina
Mavugo imefunga sita tu; Mavugo matatu, Ajibu mawili na Blagnon moja.
Yaliyobaki matano yamefungwa na Kichuya na mawili yamefungwa na Jamal Mnyate.
Hata hivyo, kwa muda sasa Mavugo amekuwa gumzo
kutokana na kushindwa kutumia nafasi au kuelewana vyema na wenzake wanapopata
nafasi za kufunga, licha ya kufunga katika mechi tatu mfululizo za awali, sasa
ana rekodi mpya ya kutofunga mechi nne mfululizo za mwisho za Simba.
Katika michezo hiyo minne, Mavugo alifanyiwa mabadiliko
katika michezo mitatu mfululizo, mechi waliyocheza na Azam, alitoka na nafasi
yake kuchukuliwa na Blagnon, akafanyiwa mabadiliko pia walipovaana na Majimaji
na kuingia Mohammed Ibrahim ‘Cabaye’, mechi ya mwisho ilikuwa dhidi ya Yanga
alipompisha tena Blagnon.
Post a Comment