DAKIKA 90 za watani wa jadi zilimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na presha kubwa kwa waamuzi wa mchezo huo, Martin Saanya mwamuzi wa kati, Samwel Mpenzu, Ferdinand Chacha na Elly Sasii  kushindwa kumudu na kwenda na kasi ya mchezo huo.
Mchezo huo uliotawaliwa na ubabe mwingi kwa wachezaji kuchezeana rafu, kama waamuzi hao wangekuwa makini hapana shaka zilitakiwa kuonyeshwa kadi zaidi ya tatu zilizoonyeshwa katika mchezo huo.
Saanya alishindwa kumudu pambano hilo, hata kushindwa kumwonyesha kadi nyekundu mchezaji sahihi aliyemsukuma wakati wakizongwa na wachezaji wa Simba, kupinga bao la Tambwe.
Mtu sahihi aliyepaswa kupewa kadi nyekundu katika tukio lile ni Ibrahim Ajib, aliyemsukuma na si Nahodha Jonas Mkude, aliyepewa kadi.
Kama angekuwa makini tungeshuhudia Novaty Lufunga pia  akipewa kadi nyekundu katika dakika ya 54 kwa mchezo  usio wa kiungwana dhidi ya Amis Tambwe.
Juma Abdul, kama mwamuzi angekuwa makini alipaswa kutolewa kwa kadi nyekundu mara baada ya kumchezea  madhambi  Mwinyi Kazimoto mara sita katika dk ya 3, 8, 44, 15, 54 na ya 51.
Kitendo cha utovu wa nidhamu walichokifanya  washambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma dakika ya 53 pamoja na Amis Tambwe dakika 48 cha kuutupa  mpira wakati imeamuliwa ipigwe faulo walipaswa kuonywa na mwamuzi huyo, lakini badala yake mwamuzi aliacha tukio hilo.

Mwamuzi huyo alishindwa kuumudu mchezo huo ambapo dakika ya 63 yeye pamoja na msaidizi wake walipishana katika maamuzi, mara baada ya madhambi aliyochezewa Juma Mahadhi na kisha mpira kuelekea upande wa Yanga.
Mpaka dakika tisini za mchezo huo zinamalizika, mwamuzi huyo alikuwa ametoa kadi tano za njano na moja nyekundu.
Si mara ya kwanza kwa Saanya kukumbwa na misukosuko katika mchezo unaoihusisha Yanga. Mwaka 2013 yeye na  msaidizi wake namba moja, Jesse Erasmo, waliochezesha mechi kati ya Yanga na Coastal Union, iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, walifungiwa mwaka mmoja.

Post a Comment

 
Top