WAKATI Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu
Nchemba, akimwita faragha Amissi Tambwe wa Yanga, bao lililofungwa na
mshambuliaji huyo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba
mwishoni mwa wiki iliyopita, limezidi kutetewa hadi huko Ulaya.
Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kuumiliki mpira mrefu
uliorushwa kutoka katikati ya uwanja na Mbuyu Twite, huku ikidaiwa
aliusindikiza kwa mkono mpira huo kabla hajautia kimiani na kumwacha kipa
Vincent Angban akiwa hana la kufanya.
Tambwe alisema kikao chake na Waziri
huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, ni cha kawaida
kikihusu masuala yao binafsi.
“Nipo njiani naelekea mjini kukutana na
Mheshimiwa Waziri Nchemba kuzungumza mambo ya kawaida tu,” alisema Tambwe huku
akionekana kuwa na furaha isiyo kifani kwa kupata fursa hiyo adimu.
Wakati hayo yakiendelea Dar es Salaam,
mtandao wa www.dailycannon.com umelitetea bao la Arsenal lililofungwa na
Laurent Koscielny dakika za lala salama kwa mkono wakati wa mchezo wa Ligi Kuu
England dhidi ya Burnley, ambalo limeonekana kuzua utata miongoni mwa wapenzi
wa soka duniani kote kama ilivyokuwa kwa bao la Tambwe la Jumamosi ya Oktoba
mosi.
Mtandao huo umeungana na mwamuzi wa
zamani, Dermot Gallagher ambaye amesisitiza kuwa bao la Koscielny alilofunga
Jumapili iliyopita, lilikuwa halali japo mazingira yake yalionekana kuwa tata
zaidi kuliko hata ilivyokuwa kwa lile lililowekwa kimiani na Tambwe.
Mtandao huo umesema kuwa ili iwe faulo,
lazima kuonekane dhamira ya makusudi ya kuunawa mpira au kuuzuia kwa namna
yoyote ile na si mpira uufuate mkono.
“Sheria za mchezo zinasema kuwa ni
lazima mtu awe ameushika mpira kwa makusudi ili ihesabike faulo,” unasema
mtandao huo.
Kama ilivyokuwa kwa Koscielny, Tambwe
naye alionekana wazi kutokuwa na dhamira ya kuushika mpira uliopigwa kwake na
Twite ambapo baada ya kumzidi ujanja Lufunga, ‘alijitengea’ kwa kifua na mpira
huo kumparaza mkononi kabla ya kutua chini na mkali huyo kumchagua kipa wa
Simba, Vincent Angban na kucheka na nyavu.
Kwa maelezo ya mtandao huo, kuna
utofauti kati ya kuushika mpira kwa makusudi ili kubadili mwelekeo wake na
mpira kubadili mwelekeo baada ya kugonga mkono wa mchezaji husika kama
ilivyokuwa kwa Koscielny na Tambwe.
Katika kuongezea hilo, tulimtafuta mmoja
wa waamuzi makini nchini ambaye alisema: “Kwa mazingira kama yale, mwamuzi
hawezi kupiga filimbi kirahisi labda kama ana tatizo kwani kama ni huyo Tambwe,
tayari alishamwacha yule beki wa Simba aliyekuwa akimkaba, hivyo hata kama ule
mpira usingemgonga mkononi, angefunga tu.”
Katika mchezo huo wa watani wa jadi
ambao mwamuzi wa kati alikuwa ni Martin Saanya, timu hizo zilitoka sare ya bao
1-1, ikiwa ni baada ya winga wa Simba, Shiza Kichuya, kusawazisha bao dakika ya
87.
Post a Comment