NAHODHA na
kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude, amepongeza maamuzi ya Kamati ya Bodi ya
Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kutengua adhabu yake ya kadi nyekundu
aliyoipata katika mechi dhidi ya Yanga, Jumamosi iliyopita.
Mkude amesema
kadi hiyo aliyopewa na Martin Saanya ilikuwa ikimtesa na kumnyima raha kwa kuwa
hakufanya kitendo kilichodaiwa kuwa alikifanya na kudai kuwa kilichotokea ni
kumfedhehesha kwa kiwango cha juu kwa kumsingizia kosa ambalo hakufanya.
Kadi ya Mkude
ilidaiwa kuwa ilitokana na kumsukuma mwamuzi huyo wakati akilalamikia bao
lililofungwa na Amissi Tambwe.
“Ile kadi ilinifedhehesha
sana na kuniweka katika wakati mgumu na kunitesa, nilikuwa nawaza kila siku juu
ya mashabiki kuwa wananifikiriaje, ilionekana nimesababisha timu ikacheza
pungufu, nilijua sijafanya kosa hilo kwa kuwa sikumgusa mwamuzi hata kidogo na
ndiyo maana nikawa na hasira.
“Ifike hatua
pindi itakapofika mechi kubwa kama hizi waletwe waamuzi kutoka nje ya Tanzania
ili kuweza kuchezesha kwa kuondoa utata kama huu kwani kadi niliyopewa mimi ni
wazi nimeonekana kuigharimu timu katika mchezo ule kwa kucheza pungufu.
“Nilitamani
nipate mkanda wa tukio lile siku ileile baada ya mchezo kwisha niwaonyeshe
Watanzania ili waone juu ya kile kilichotokea, lakini nimefurahishwa na maamuzi
ambayo yananitia faraja sana ambayo yamefanya ukweli ujulikane na mashabiki wa
Simba wafahamu ukweli juu ya hilo,” alisema Mkude.
Post a Comment