KAMATI ya Bodi ya
Ligi Uendeshaji na Usimamizi umeipiga faini klabu ya Simba ya shilingi milioni
tano na kuiagiza ilipe fedha za ukarabati wa viti kutokana na uharibifu uliofanywa na mashabiki
wa timu hiyo wakati wa mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya mahasimu wao
Yanga mtanange uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba
mosi.
Kamati hiyo
iliyoketi jana imemuondolea adhabu ya kadi nyekundu kwa nahodha wa timu ya
Simba Jonas Mkude baada ya kujiridhisha bila mashaka kuwa mchezaji huyo
hakustahili kupewa kadi hiyo.
Mbali na ripoti
ya kamishna wa mchezo huo uliooneshwa moja kwa moja kwenye luninga kamati inaendelea na uchunguzi
kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi Martin Saanya na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na
Ferdinand Chacha kabla ya kutoa maamuzi mengine dhidi yao endapo itathibitika
kuwa walifanya makosa kwenye mchezo huo.
Ofisa Habari wa
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema Kamati hiyo
inaendelea na uchunguzi kuhusu mechi mbali mbali za ligi kuu na kuzitolea
maamuzi ya haraka.
"Kumekuwa na
taarifa za upotoshaji zinatolewa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hilo
la mechi ya Simba na Yanga, lakini hii ndiyo rasmi kutoka ndani ya kamati"
alisema Lucas.
Kamati hiyo pia
imempiga faini Msemaji wa klabu ya Simba Hajji Manara ya shilingi laki mbili
kwa kosa la kuingia uwanjani licha ya kutokuwa miongoni mwa maofisa waliotakiwa
kuwepo eneo hilo.
Wakati huo huo
klabu ya Azam imepigwa faini ya shilingi milioni tatu baada ya kuvaa nembo ya
mdhamini wa ligi mkono mmoja badala ya miwili kwa mujibu wa kanuni za ligi.
Boiplus
Post a Comment