SIMBA
haitaki mchezo! Wekundu hao wa Msimbazi wamejipanga kufanya kile ambacho
mashabiki wao wanakihitaji na kwa kuanzia wamepanga kufanya usajili
utakaotingisha nchi.
Unajua
ikoje! Baada ya kuanza mazungumzo na straika wao wa zamani Mganda, Emmanuel
Okwi ili kumrudisha dirisha dogo la usajili, vigogo hao wamemfungia kazi
mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche.
Taarifa za
uhakika kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa mbali na Okwi na Kipre, Wekundu hao
wa Msimbazi wameanza mpambano wa kumrejesha beki wao wa zamani, Shomari
Kapombe, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Azam FC.
Kuhusu Okwi,
taarifa zinadai mazungumzo yanakwenda vizuri na suala lake haliwaumizi sana
kichwa Wekundu hao wa Msimbazi, kwani hana namba katika kikosi chake cha sasa
cha SonderjyskE, kinachoshiriki Ligi Kuu nchini Denmark.
Taarifa
zaidi kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa kwa upande wa Kipre, ambaye anakipiga
nchini Oman, wamepania kufanya kila linalowezekana ili kumng’oa na kwa jinsi
Wekundu hao wa Msimbazi walivyojipanga, zoezi hilo linaweza kufanikiwa.
Kwa upande
wa Kapombe, Wekundu hao wa Msimbazi wameendelea kuvutiwa na uwezo wake, ambapo
wanaamini atakuwa msaada mkubwa na sasa wametega mitego kila kona kuhakikisha
nyavu zao zinamnasa beki huyo, ambaye aliwahi kuichezea Simba.
Jeuri ya
Simba ya kutaka kuwasajili Okwi, Kipre pamoja na Kapombe kwa wakati mmoja
inatokana na kujitoa kwa hali na mali kwa mfanyabiashara maarufu na Mwanachama
wao, Mohamed Dewji ‘MO.’
Dewji,
ambaye kwa sasa anasubiri tu kukabidhiwa timu kutokana na kutaka kuweka hisa ya
asilimia 51, amekuwa akimwaga fedha, zikiwamo zile za mishahara kwa wachezaji,
akisaidiana na matajiri wengine na uongozi chini ya Rais Evance Aveva.
Kigogo mmoja
ndani ya Simba aliliambia DIMBA kuwa baada ya kuteseka kwa miaka minne
mfululizo, sasa wamejipanga kwa kila hali kuhakikisha wanafurahi kwa kutwaa
ubingwa na kushiriki michuano ya kimataifa.
“Hayo yote
yanayofanyika ni ili kurejesha furaha yetu ambayo imepotea kwa miaka minne
mfululizo, uongozi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, akiwamo Mohamed Dewji,
wameamua kufanya makubwa sana msimu huu,” alisema kigogo huyo.
DIMBA
lilimtafuta Kipre Tchetche ili kuzungumzia suala hilo, ambapo alisema tetesi
hizo zilianza kuenea hata kabla ya kwenda Oman na kwamba kwa sasa
anachokiangalia ni kufanya kazi na timu ambayo anaitumikia.
“Sishangai
kusikia hivyo, kwani mchezaji yeyote kuhusishwa na timu nyingine ni jambo la
kawaida, taarifa hizo kama unakumbuka zilianza kuenea hata kabla ya mimi kuja
huku Oman, ila niseme tu naendelea kuitumikia timu yangu mpya huku niliko,”
alisema.
Kwa upande
wa Okwi, alisema hawezi kuzungumzia suala lolote la kurejea Simba, kwani ana
imani Simba ni klabu ambayo ilimfanya ajulikane.
“Simba ni
timu ambayo imenilea na tetesi za kurudi kuichezea tena zimekuwepo kwa muda
mrefu, kwa sasa sitasema chochote,” alisema Okwi.
Post a Comment