MWENYEKITI wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara (Fam), Michael Wambura ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba, ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi ya kesho ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Azam FC.
Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana ilimtangaza Wambura kuwa kamishna wa mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Pia mwamuzi Israel Nkongo ambaye alishushiwa kipigo na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo dhidi ya Azam mwaka 2012, ametangazwa kuwa mwamuzi wa kati wa mechi hiyo ya kesho.
Nkongo mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ambaye kitaaluma ni mwalimu wa sekondari, atasaidiwa na Soud Lila na Frank Komba huku mwamuzi wa mezani akiwa Helen Mduma wote wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Tanzania (Frat), Nassor Mwalim, alisema: “Jukumu la kumteua kamisaa ni la Bodi ya Ligi ila lina vigezo vyake.
“Anatakiwa kuwa mwadilifu, mwaminifu na awe anatokea kwenye familia ya soka, kwa maana ya kuwa ni mchezaji wa zamani au mwamuzi wa zamani au aliwahi kuongoza soka.”
Katika mchezo wa ligi kuu wa Simba na Kagera Sugar leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, mwamuzi atakuwa Hussein Athumani wa Katavi akisaidiana na Joseph Bulali (Tanga) na Sylvester Mwanga (Kilimanjaro) na mwamuzi wa mezani ni Soud Lila. Kamishna atakuwa Pius Mashela wa Dar es Salaam.



Post a Comment

 
Top