KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesikia baadhi ya watu
wakisema Simba ndio watakaotwaa ubingwa msimu huu kutokana na kasi waliyonayo
akatabasamu kidogo, kisha akatamka wazi kuwa hakuna wa kuwapoka ubingwa wao.
Mabingwa hao watetezi watashuka katika Dimba la CCM Kirumba jijini
Mwanza leo Jumatano kuwakabili Toto African, ikiwa ni mfululizo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, mchezo ambao Wanajangwani hao wamepania kushinda.
Katika msimamo wa ligi hiyo, mabingwa hao watetezi wanashika
nafasi ya tatu wakiwa na pointi 15, kutokana na michezo saba waliyocheza, huku
watani zao wa jadi, Simba, wakiwa kileleni na pointi zao 23, wakicheza michezo
tisa na Stand United nafasi ya pili na pointi zao 20 wakiwa wamecheza michezo
20.
Pluijm amesema kuwa, mtu ambaye anaitoa Yanga kwenye mbio za
ubingwa anakosea, kwani mabingwa hao watetezi wanajua nini wanakifanya na baada
ya ligi kumalizika ndiyo mbivu na mbichi zitajulikana.
“Nikiri kwamba hata wapinzani wetu wamejipanga vizuri na msimu huu
ni tofauti na msimu uliopita, ila kuhusu mbio za ubingwa sisi Yanga tunatambua
jukumu letu na tunaendelea kusisitiza kuwa tutatetea ubingwa wetu,” alisema.
Akizungumzia kelele za baadhi ya mashabiki kwamba kikosi hicho kwa
sasa kimechoka ndiyo maana hakipati matokeo mazuri kwa asilimia 100% kama
kawaida yao, alisema hayo ni mawazo yao na hawezi kuwapinga, ila wajue kwamba
huu ni mpira.
“Kwanza nikiri kwamba sisi tumetumika sana kuanzia Ligi ya msimu
uliopita na michuano ya kimataifa, huku baadhi ya wachezaji wangu wakijumuishwa
kwenye timu zao za Taifa.
“Kwa
ujumla hatujapata muda wa kupumzika, kwani tulipomaliza michuano hiyo ya
kimataifa na ligi ikaanza, sasa hapo utaona mwenyewe jinsi mambo yalivyo, hata
hivyo, niwahakikishie mashabiki wetu kwamba, tunaendelea kupambana mpaka tone
la mwisho,” alisema.
Post a Comment