KATIKA hali isiyokuwa ya
kawaida, juzi beki na nahodha msaidizi wa Yanga raia wa Togo, Vincent Bossou
alimfuata mshambuliaji wa Simba nje ya uwanja Mrundi, Laudit Mavugo na
kumchimba mkwara mzito.
Tukio hilo la aina yake
lilitokea wakati watani wa jadi, Simba na Yanga, walipovaana wikiendi kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
Ishu ilikuwa hivi, timu hizo
zikiwa katika maandalizi ya mchezo huo wa Ligi Kuu Bara wakati kila moja
ilipoweka kambi yake Yanga huko Pemba na Simba mkoani Morogoro, Mavugo alitamba
kupita mbele ya Bossou na kufunga mabao.
Taarifa hizo, zilionekana
kumkera Bossou na kupanga kupambana na Mavugo kwa kuzunguka naye kila kona ya uwanja
kwa ajili ya kuzuia mipango yake hiyo.
Wakati wa mechi hiyo, Bossou
alionekana kufanikiwa kwa kiwango kikubwa akisaidiana na Kelvin Yondani kwa
kutompa nafasi ya kumiliki mpira mshambuliaji huyo hadi pale alipotolewa dakika
62 na nafasi yake kuchukuliwa na Frederick Blagnon.
Mavugo akiwa anatoka nje ya
uwanja, Bossou alikimbia kutoka nyuma golini kwao na kuanza kumchimba mkwara
kwa maneno na vitendo huku akimcheka na kumtaka kwa ishara acheze soka na siyo
kuongea, aliendelea kumchania mbovu hadi alipokwenda kukaa kwenye benchi la
Simba.
Mara baada ya mechi hiyo
kumalizika Championi Jumatatu lilimfuata Bossou na kumuuliza sababu ya
kumchimba mkwara Mavugo, akasema: “Yeye si alisema hanihofii na atatupita mabeki
wa Yanga na kufunga mabao, haya kipo wapi, mbona katolewa nje bila ya kutufunga
na kikubwa alichokifanya ni kipi katika mechi hii? Nimwambie tu, mimi
nimekabana na washambuliaji wengi wakubwa kutoka mataifa mbalimbali wengine
wanacheza soka Ulaya akina Drogba (Didier) wa Ivory Coast, itakuwa yeye?”
Post a Comment