SIKU chache baada ya BINGWA kufichua taarifa kuwa klabu ya Yanga inakaribia kumnasa kocha wa Zesco, Mzambia George Lwandamina, ghafla zimeibuka stori kuwa Azam wanasubiri miamba hiyo ya Jangwani ijichanganye kumtimua kocha huyo ili wao wampeleke Chamazi.
Taarifa hizo zinadai kuwa jina la Pluijm liko kwenye akili za viongozi wa Azam ambao wameanza kuchanganywa na kufanya vibaya kwa timu yao kwenye mechi zake kadhaa za msimu huu.
Kutokana na kuzinasa taarifa hizo, BINGWA bila hiyana liliamua kuingia chimbo na kutafuta ukweli juu ya hayo yanayosemwa na mashabiki na wadau wa soka nchini kuhusiana na Azam kumvizia Pluijm.

 Hivyo, BINGWA liliwasiliana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, ili kupata ukweli juu ya taarifa hizo ambazo zimeanza kuenea miongoni mwa mashabiki wa soka nchini.
Kawemba aliliambia gazeti hili kwa sasa hawana mpango na kocha huyo kwa sababu benchi lao la ufundi lipo kamili na wanaamini baada ya muda kikosi chao kitarudia makali yake ya misimu iliyopita.
Mtendaji huyo alisema nafasi ya kocha siku zote ni moja na tayari wana kocha wao na hawajawahi kufikiria kumchukua Pluijm kwa sababu hata akienda kwenye timu hiyo hawana pa kumweka.

Post a Comment

 
Top