SAA chache baada ya kuripotiwa
kujiuzulu, imeripotiwa kuwa aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, yuko
katika rada za Azam FC ambao inadaiwa kufanya naye mazungumzo ya siri.
Pluijm alimaliza majukumu ya kuinoa
Yanga Jumatatu kisha akaandika barua ya kujiuzulu punde tu alipobaini Yanga
imefanya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina.
Taarifa
za uhakika kutoka ndani ya Azam, zinasema kuwa klabu hiyo ya Chamazi imekuwa
ikifanya mchakato wa chini kwa chini yakiwemo mazungumzo na uongozi tangu
iliporipotiwa kuwa Yanga wako mbioni kumtema.
Chanzo
chetu cha habari kimeeleza kuwa Pluijm alilifahamu mapema suala la yeye
kutakiwa kuondolewa kwenye benchi la ufundi la Yanga, hivyo akaamua kuzungumza
na matajiri hao wa Ligi Kuu Tanzania ambapo walifikia mwafaka.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, hata baada
ya Yanga kuwasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita ikitokea Kanda ya Ziwa,
wajumbe wawili wa Azam walikwenda uwanja wa ndege na kumchukua kocha huyo kisha
wakaenda naye mafichoni kuzungumza naye.
Inasemekana kwamba uamuzi wa Azam
kutaka kumchukua Pluijm unatokana na ukweli kwamba klabu hiyo imekuwa haifanyi
vizuri tangu kuanza kwa msimu huu ambapo imekuwa chini ya kocha Mhispania,
Zeben Hernandez na msaidizi wake.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa bado
haijajulikana iwapo kocha huyo Mholanzi atachukua nafasi ya kocha mkuu au kuwa
mkurugenzi wa ufundi, lakini taarifa nyingine zinadai kwamba katika mipango ya
klabu hiyo huenda kocha Mhispania Hernandez na msaidizi wake watahamishiwa
katika kituo cha vijana cha klabu hiyo ili kuendeleza na kukuza vipaji kwa vile
bado wana mikataba nao.
DIMBA Jumatano lilifanikiwa kuzungumza
na Pluijm ambaye alikiri kupata ofa nyingi lakini hakutaka kuweka wazi ni timu
gani ambazo zinamhitaji.
Alisema analifahamu vizuri soka la
Afrika pamoja na kuwa na uzoefu mkubwa na ana imani hawezi kukosa timu, kwani
kuna timu nyingi ndani na nje ya Tanzania zinahitaji huduma yake.
“Nimejifunza vitu vingi nikiwa hapa
nchini, pia Yanga wanaweza kuleta mtu wanayemtaka lakini kikubwa ni kwamba
mlango mmoja ukifungwa, mwingine hufunguliwa,” alisema Pluijm.
Jana asubuhi, Pluijm huku akiwa
amevalia ‘mkanda nje’, alikwenda kuwaaga wachezaji wa Yanga na kuzungumza nao
kwa muda kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi,
Kurasini, Dar es Salaam na akawatakia kila la heri chini ya kocha mpya ajaye.
Akitoa nasaha zake, Pluijm amewaasa
wachezaji kuendelea kujituma na kufanikisha azma yao ya kutetea taji lao kwa
mara nyingine, kudumisha nidhamu, kupendana na kutanguliza mbele masilahi ya
timu kuliko masilahi binafsi.
Pluijm pia aliagana na wasaidizi wake
Juma Mwambusi, anayeiongoza timu kwa sasa, kocha wa makipa, Juma Pondamali,
Meneja Hafidh Saleh, mtunza vifaa vya timu, Mahmoud Omar ‘Mpogoro’ na daktari
wa timu, Edward Bavu.
Post a Comment