MSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu, ametoweka
katika kikosi hicho baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Simba huku akiwa
hajatoa taarifa yoyote kwa uongozi wa klabu hiyo, kisa kikidaiwa kuwa ni kukosa
nafasi ya kucheza.
Taarifa zinaeleza kuwa, mshambuliaji huyo ameamua
kutoweka kutokana na kuona hapewi nafasi katika kikosi hicho tangu msimu
ulipoanza, hivyo ameamua kujiongeza zaidi.
Chanzo kutoka Yanga kimeeleza kuwa, Busungu
alikuwa na mpango huo tangu katika mechi dhidi ya Stand United, lakini akaja
kufanya utekelezaji wake baada ya mechi na Simba ambapo aliamua kuzima simu
yake kabisa.
“Busungu alikuwa na mipango ya kuondoka tangu
tulipomaliza mechi yetu na Stand United ambapo aliamua kuondoka rasmi baada ya
kumalizika mechi na Simba, kisa kikiwa ni kukosa nafasi ya kucheza.
“Baada ya kutoweka hakuwa akipatikana na simu
yake ilikuwa imezimwa kila alipokuwa akipigiwa, hivyo kwa taratibu za kazi mtu
akitoweka kazini siku tatu bila ya mawasiliano ajira yake inakuwa ameisitisha
mwenyewe mkataba kwa kuwa hayupo klabuni zaidi ya wiki sasa,” kilisema chanzo
hicho.
Aidha Championi liliendelea kuchimba zaidi katika
benchi la ufundi ambapo lilipata taarifa kuwa mchezaji huyo amesema hawezi
kurejea kikosini hapo kwa madai kuwa ana matatizo ya kifamilia nyumbani kwao Tanga
ikiwa ni pamoja na kuumwa.
“Hivi karibuni simu yake ilipatikana na nimeongea
naye lakini amesema hawezi kurejea kwa sasa kufanya mazoezi na Yanga kwa kuwa
bado anaumwa, pia ana matatizo ya kifamilia ambayo yanamzuia kuja kujiunga na
timu.
“Ameondoka bila ya kuaga na tayari barua
imeshafikishwa kwa uongozi juu ya kufanya maamuzi yake kwani hata benchi la
ufundi limeshindwa kutoa maamuzi yoyote,” kiliongeza chanzo kingine.
Hata hivyo, alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga,
Baraka Deusdedit, amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema: “Ni kweli
jambo hilo lipo lakini lipo kiofisi zaidi na aliomba ruhusa na iwapo kuna watu
wanasema hajaomba ruhusa basi waulize haohao.”
Alipotafutwa Kocha wa Yanga, Hans Pluijm
kuzungumzia juu ya suala hilo, alisema: “Busungu ana matatizo binafsi ambayo
yatatatuliwa ndani ya uongozi, hivyo siwezi kuzungumzia.”
Alipotafutwa Busungu kuweza
kuzungumzia suala hilo simu yake ilikuwa inaeleza inatumika kila wakati na hata
alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.
Post a Comment