Wekundu hao jana waliendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kama kawaida, winga machachari wa timu hiyo, Shiza Kichuya, aliendelea kudhihirisha kwamba yeye ni nyota wa kuogopwa msimu huu baada ya kufunga bao moja kati ya mawili huku akimtengenezea jingine Mzamiru Yassin.
Wekundu hao wa Msimbazi walianza kujipatia bao la kwanza katika dakika ya 43 kipindi cha kwanza kupitia kwa Mzamiru, ambaye alifunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Kichuya kutoka Kaskazini Mashariki mwa uwanja.
Simba ilipata bao la pili kwa njia ya penalti baada ya Mohamed Ibrahim, aliyekuwa ameingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib, kufanyiwa madhambi eneo la hatari na mwamuzi kuashiria penalti ambayo ilifungwa kiufundi na Kichuya na kufikisha idadi ya mabao saba.
Awali mpira huo ulianza kwa kasi kubwa huku wachezaji wa pande zote wakicheza kwa tahadhari kubwa kuepuka kufungwa bao la mapema, huku eneo la katikati mwa uwanja likitawaliwa na ufundi mwingi kwa pande zote.
Simba walifanya shambulizi kubwa katika dakika ya 18 ya mchezo huo ambapo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alipiga mpira mzuri wa kona kutoka winga ya kushoto, Frederick Blagnon, akaunganisha kwa kichwa lakini kipa wa Kagera akauona na kuuokoa kwa ufundi mkubwa.
Wakati mashabiki wakidhani dakika 45 za kipindi cha kwanza zitamalizika timu hizo zikiwa 0-0, ndipo Kichuya alipochonga kona maridhawa iliyotua kwenye kichwa cha Mzamiru na kujaa moja kwa moja wavuni ikimwacha kipa wa Kagera Sugar, Hussein Shariff ‘Cassilas’, akishindwa kujua la kufanya.
Katika dakika ya 45, Jonas Mkude, alitoa pasi nzuri akiwa katikati ya uwanja na kumkuta Kichuya ambaye aliachia shuti kali lililotoka sentimita chache kwenye lango la Kagera Sugar na kuzifanya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika Simba wakiongoza kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kagera Sugar kupeleka mashambulizi kwa Simba ambapo katika dakika ya 52, Ally Nassor aliachia shuti lakini kipa Vincent Angban akaudaka.
Simba walifanikiwa kujipatia bao la pili katika dakika ya 75 kupitia kwa Kichuya kwa njia ya penalti ambapo hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika wakaibuka na ushindi huo wa mabao 2-0.
Kwa matokeo hayo, Simba wanaendelea kukalia usukani wa ligi baada ya kufikisha jumla ya pointi 23 wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kati ya michezo tisa ambayo wamecheza mpaka sasa.
Katika mchezo huo, Simba iliwakilishwa na Vincent Angban, Jarvie Bukungu, Mohamed Hussein, Juuko Murushid, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Frederick Blagnon/Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib/Mohamed Ibrahim, na Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla.
Kagera Sugar wao waliwakilishwa na Hassan Shariff ‘Cassilas,’ Godfrey Taita, George Kavilla, Mwaita Gereza, Juma Ramadhan, Seleman Maongoma, Ally Nassor, Shaban Sunza, Dan Mrwanda/Themi Felix, Christopher Edward/Paul Ngwai, pamoja na Mbaraka Abeid.
Katika michezo mingine iliyopigwa hiyo jana, Mwadui FC ilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya JKT Ruvu, Stand United ikatoshana nguvu na African Lyon.
Leo Jumapili Yanga itakipiga na Azam FC Uwanja wa Uhuru, Ruvu Shooting itaikaribisha Mbeya City Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Toto Africans itakuwa mwenyeji wa Majimaji Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.

Post a Comment

 
Top