HIVI sasa makocha mbalimbali wameanza kumwaga sifa kwa kikosi hicho. Baada ya Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, kuimwagia sifa klabu hiyo wiki iliyopita, juzi Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa ‘Master’ amekiri Simba ya msimu huu ni moto wa gesi na kuongeza kuwa ina sababu zote za kuweza kufanya vizuri zaidi, ikiwezekana kuchukua ubingwa, lakini akasisitiza sana juu ya fowadi yake.
Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, aliyasema hayo baada ya kuishuhudia Simba ikichomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar, juzi Jumamosi.
 “Simba ina kikosi kizuri, karibu imekamilika kila idara, kuanzia golini mpaka kiungo iko vizuri sana na inacheza kwa kuonana, lakini sema bado wana tatizo kwenye safu ya ushambuliaji. Wapo baadhi wanakwamisha mbinu za mwalimu, wanaonekana kila mmoja anataka afunge mwenyewe hata kama hayupo kwenye nafasi ya kufunga. Hili ndilo tatizo kubwa kwa timu yao. Sitawataja lakini wapo na ni tatizo kwa timu yao.

“Nafikiri kocha wao akifanikiwa kulitatua, iwe ni kuelewana ama kukemea naamini Simba inaweza kufanya kitu cha ajabu msimu huu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Ruvu Shooting.
Licha ya kutowataja lakini tunafahamu aliwalenga zaidi Fredric Blagnon na Laudit Mavugo ambao mara kadhaa kumekuwepo na malalamiko juu yao kwa umimi kama ilivyotokea kwenye mchezo wa juzi.
Ushindi huo uliifanya Simba iendelee kung’ang’ania kileleni kwa kufikisha pointi 23 huku kichapo kikiiacha Kagera na pointi zao 13.

Post a Comment

 
Top