WAKATI mashabiki wa Yanga wakiduwazwa na kiwango cha juu alichokionyesha mchezaji, Haruna Niyonzima, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Toto Africans, kiungo huyo amefunguka na kusema anafurahia zaidi uamuzi wa kocha wake, Hans Van Der Pluijm wa kumpanga kucheza kiungo wa kati (namba nane) kuliko akicheza winga.
Niyonzima alisema anakuwa huru uwanjani akicheza nafasi hiyo kutokana na ukweli kwamba inamuweka katika nafasi nzuri zaidi ya kusambaza mipira kwa wakati na kuiunganisha timu.
“Unajua mimi napenda sana kucheza katikati ila kwa sababu kocha ndio bosi wa kila kitu, sina budi kumsikiliza lakini nimefurahi sana alipoamua kunipanga sehemu ambayo nimeicheza kwa miaka mingi,” alisema Niyonzima.
Alisema hapendi kuingilia masuala ya kiufundi ya benchi la ufundi la timu hiyo na kulazimisha apangwe nafasi hiyo, isipokuwa ameamua kiroho safi kucheza nafasi yoyote atakayopangwa uwanjani.
Kiungo huyo wa kutumainiwa wa Yanga na timu ya Taifa ya Rwanda, juzi alionyesha kiwango kikubwa katika mchezo dhidi ya Toto na kuwafanya mashabiki kumfurahia.
Niyonzima aliripotiwa kuwa na mgogoro na kocha wake Pluijm, kutokana na madai ya kushuka kiwango ambapo inaelezwa kwamba Pluijm alimtaka nyota huyo kukuza kiwango chake, la sivyo angeendela kukalia benchi.
Post a Comment