NAHODHA wa Simba, Jonas Mkude,  ameuza siri za Simba baada ya kusema kwamba ushindi wanaoupata katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatokana na umoja wa wachezaji na viongozi wa klabu hiyo.
Mkude alisema licha ya kiwango kizuri kinachoonyeshwa na wachezaji, lakini umoja unachangia  kupata ushindi kwa timu yao.
Mkude alisema baada ya kukosa ubingwa kwa muda mrefu imewafanya kila mchezaji kutambua deni lake kwa mashabiki wa klabu hiyo na kuwafanya wajitume kwa nguvu zote wanapokuwa uwanjani.
“Kikubwa kinachoifanya timu yetu ibadilike msimu huu ni umoja uliokuwepo wa wachezaji na ili tuendelee kufanya vizuri umoja huu usivunjike.
“Nadhani wachezaji wote wanajua deni  linalotukabili ni kukaa muda mrefu bila ubingwa, lazima tupambane tuweze kulipa,” alisema Mkude.
Kikosi cha Simba
Mkude alisema mipango waliyojiwekea ni kucheza kila mechi kama fainali bila kujali timu wanayokutana nayo wala mahali wanapocheza.
Alisema katika mechi yao ya leo  itakayochezwa kwenye Uwanja wa  Uhuru, Dar es Salaam dhidi ya Mbao  wamejipanga kuibuka na ushindi ili waendelee kukaa kileleni.
Mkude alisema hawataidharau timu hiyo kutokana na uchanga wao kwenye ligi hiyo, kwani watakachohitaji ni kuona wanaondoka na pointi tatu.
Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi kutokana na pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa, wakishinda saba huku wakitoka sare mbili.

Post a Comment

 
Top