NOMA sana, ndiyo kauli unayoweza kuitumia baada ya kuuona mkataba ambao klabu ya Yanga imeingia na Kampuni wa Yanga Yetu Limited inayomilikiwa na bilionea mmoja nchini wa kuikodisha nembo ya timu hiyo kwa kipindi cha miaka 10.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo BINGWA iliipata jana kutoka kwa Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, imeamua kuyafanyia kazi makubaliano ya kukukodisha nembo ya klabu hiyo yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Dharura wa klabu hiyo uliofanyika Agosti 6 mwaka huu.
Ilipitishwa kuwa nembo ya klabu hiyo ikodishwe kwa miaka 10 na makubaliano yalikuwa asilimia 75 zichukuliwe na mkodishwaji ambaye sasa ni Kampuni ya Yanga Yetu Limited huku asilimia 25 zikibaki kwa wanachama wa klabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Wadhamini wa Yanga, tayari mkataba wa kuikodisha timu hiyo umeingiwa Septemba 3, 2016, huku mkataba huo ukiwa umetazama nyanja mbalimbali za kiuendeshaji ambazo zimelenga kuinufaisha klabu hiyo.

Deni
Kutokana na timu ya Yanga kujiendesha kwa hasara kwa kipindi kirefu, timu hiyo ilijikuta kwenye deni la shilingi bilioni  11.676, ambalo lilitokana na gharama mbalimbali za uendeshaji wa timu kama kulipa mishahara wachezaji, usajili, posho na gharama za usafiri.
Lakini kwa mujibu wa taarifa ya muhtasari wa mkataba iliyotolewa jana na Bodi ya Wadhamini, deni hilo si tatizo tena kwa klabu hiyo ya Jangwani kwa sababu litalipwa na kampuni ya Yanga Yetu Limited ambayo itaikodi klabu hiyo.

Kuimarisha matawi
Muhtasari wa mkataba wa mkataba kati ya Yanga na kampuni ya Yanga Yetu Limited, unaonesha kuwa klabu hiyo imepania kuimarisha matawi yake ambapo kwenye mkataba huo kuna kipengele ambacho kinaonyesha kuwa kampuni hiyo itailipa klabu hiyo kiasi cha shilingi milioni 100 kila mwaka ambapo asilimia 90 ya fedha hizo zitatakiwa kuwekezwa kwenye kuimarisha matawi ya klabu.

 
Kujenga uwanja
Katika kuhakikisha kuwa Yanga inakuwa na uwanja wake, kampuni hiyo inayoikodi klabu hiyo itakuwa ikiilipa kwa fedha taslimu asilimia 25 ya faida ambayo itapatikana na fedha hiyo itaelekezwa kwenye ujenzi wa uwanja wa timu hiyo.
Lakini pia mkataba huo unaonyesha kuwa siku 90 baada ya makubaliano kampuni ya Yanga Yetu Limited itatakiwa kuanza kuwekeza kwenye vitega uchumi vya klabu ikiwemo kujenga kiwanja cha mafunzo.
Pia mkataba huu umeweka wazi kuwa kampuni hiyo itatakiwa kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha inaongeza ardhi inayohitajika katika makao makuu yake yaliyopo mtaa wa Twiga ili iweze kujenga uwanja wa mpira unaofaa, kuchezea michezo yake kwa masharti yatakayokubaliwa baina ya pande zote mbili.
Mafanikio uwanjani
Pia katika kuhakikisha timu hiyo inaendelea kushiriki kwenye michuano ya kimataifa, mkataba huu umeweka bayana kuwa kampuni hiyo ambayo itaikodi Yanga inatakiwa kufanikisha timu imalize kwenye nafasi mbili za juu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania.
Soka la vijana
Katika kuhakikisha Yanga inakuwa na mfumo bora wa soka la vijana na kuzalisha wachezaji wenye mapenzi ya kweli na klabu mkataba huu unaonyesha kuwa kampuni hiyo itafadhili mashindano ya soka kwa vijana chini ya miaka 18, ambapo kila tawi la wanachama litaalikwa kutuma timu yake kushiriki mashindano hayo.
 Kuwabana wapigaji
Ili kuwabana watu ambao wanataka kuitumia Yanga kwa manufaa yao binafsi, mkataba huu unaonyesha kuwa kila mwaka kampuni hiyo italazimika kuteua moja kati ya kampuni tano za ukaguzi kongwe ulimwenguni kuja nchini kila mwaka kukagua hesabu za klabu hiyo.
Mambo ya fedha
Katika vipengele vya mkataba huo kuna sehemu inayoonyesha kuwa klabu itakuwa na haki ya kupata fedha zote zilizopatikana kabla ya kuanza kwa mkataba huu ambazo ni pamoja na shilingi milioni 300 za haki za televisheni za msimu uliopita ambazo klabu ilikuwa haijachukua TFF pamoja na fedha za zawadi, VAT kutoka TFF na fedha nyingine zote zitapewa umuhimu wa nafasi ya kwanza katika matumizi ya kukamilisha majukumu ya zamani ya klabu hiyo ambayo yalijilimbikiza na hayakuwa yamelipwa.
Mbali na vipengele hivyo kuna vingine muhimu ambavyo unaweza kuvijua kiundani kwa kuusoma muhtasari wa mkataba huo kwenye ukurasa wa tatu wa gazeti hili.

CHANZO: BINGWA

Post a Comment

 
Top