IMEBAINIKA kuwa beki wa kimataifa wa Togo anayekipiga Yanga, Vincent Bossou, aliwahi kuuomba uongozi wa mabingwa hao wa Tanzania Bara kucheza bure, ikiwa ni baada ya usajili wake ndani ya Wanajangwani hao kukumbwa na mizengwe.
Bossou alifikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwapo mipango ya kukata jina lake na kusitisha mkataba katika kipindi hicho kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Wanajangwani hao.
Mmoja wa vigogo ambaye alihusika kumsajili beki huyo, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema: “Huyu jamaa mwacheni afanye kazi jamani, kakutana na vigingi vingi sana, kapigwa vita mno, ilifikia kipindi aliuomba uongozi umpe muda zaidi au ikiwezekana acheze hata bure bila malipo yoyote ili mradi klabu impatie chakula na sehemu ya kulala tu.
“Bossou amekuja kweli kutafuta maisha hapa Tanzania, fikiria mtu anaomba apewe mahali pa kulala na kula tu, mshahara asipewe ili awaonyeshe kazi, inaonyesha jinsi alivyokuwa na uhakika na uwezo wake,” alisema.
Kigogo huyo alisema kutokana na Bossou kupita katika kipindi kigumu, ameonyesha uwezo wake na hivyo kuwafunga mdomo wale wote waliokuwa wakimbeza na kumponda na sasa kuwa kwenye orodha ya mabeki tegemeo waliopo katika kikosi Yanga.
Post a Comment