KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa, amemkingia kifua kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm na kusema  ni mapema  watu kumnyooshea vidole kutokana na mwenendo wa timu  kwa sasa.
Baada ya matokeo ya sare dhidi ya Simba  mwishoni mwa wiki iliyopita, kumekuwa na tetesi kuwa Yanga wapo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mwingine, kwa kile wanachodaiwa kuwa timu inacheza katika kiwango cha chini tangu ligi imeanza.
Mkwasa  ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Pluijm kwenye kikosi cha Yanga nchini, amekuwa akihusishwa kurejea kwenye kikosi hicho ili kuokoa jahazi.
 Akizungumza na BINGWA jana, Mkwasa alisema Yanga wanatakiwa  kumwacha Pluijm kuendelea kukinoa kikosi hicho kwa sababu bado ana nafasi ya kufanya  vizuri kulingana na michezo ya ligi iliyopo.
Alisema  michezo iliyochezwa na timu hiyo hadi sasa ni michache, hivyo fursa ipo kinachotakiwa ni kurekebisha mambo madogo ya kiufundi.
“Yanga bado ina nafasi ya kufanya  makubwa zaidi ya hapo, lakini si kwa njia ya kumuondoa kocha aliyepo, muhimu ni kufanyia marekebisho matatizo ya kiufundi yaliyoonekana katika michezo iliyopita,” alisema Mkwasa.
Kuhusu kurejea Yanga, Mkwasa alisema yupo tayari kama watakubaliana lakini  hadi amalize mkataba wake na timu ya Taifa kwa kuwa bado unambana, ila ukimalizika hakuna tatizo .
“Nashukuru kwa wadau wa Yanga kutambua na kuthamini mchango wangu, ila bado naheshimu uwepo wa kocha mwingine. Ukocha ni kazi yangu, nikimaliza mkataba na Stars, wakinihitaji na tukakubaliana, narudi Yanga hakuna shida,” alisema.

Post a Comment

 
Top