KLABU ya Fanja FC ya Oman imeijaza minoti Simba baada ya
kuipatia kiasi cha dola 10,000 (sh milioni 22) kama malipo ya usajili wa
straika wa zamani wa miamba hiyo ya Msimbazi, Danny Lyanga, aliyejiunga na
vijana hao wa Uarabuni mwishoni mwa mwezi uliopita.
Baada ya Lyanga kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea
Fanja, klabu ya Simba ilitaka kulipwa dau hilo kama ada ya uhamisho na baada ya
mvutano wa hapa na pale hatimaye Waarabu hao wametuma fedha hizo.
Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele, alisema awali Fanja
walitaka kumchukua bure Lyanga, lakini timu yake iligoma na hatimaye Waarabu
hao wakalainika na kukubali kutoa fedha hizo.
Kahemele alisema kuwa baada ya kupokea fedha hizo walitoa
dola 3,000 (sh milioni 6.6) na kumpa Lyanga mwenyewe kwa sababu bado alikuwa
akiidai klabu hiyo na kubakiwa na Dola 7,000 (sh milioni 15.4) ambazo ni faida
kwao na watazitumia kwenye mambo mbalimbali.
“Fedha za Lyanga zimeshakuja,” alisema Kahemele. “Jamaa
wamelipa dola 10,000, kati ya hizo tumempa Lyanga dola 3,000 ambazo alikuwa
anatudai kama malimbikizo ya mshahara na deni la usajili huku klabu ikipata
dola 7,000.”
Kahemele aliendelea kusema kwamba kwa kuwa Simba kwa sasa
haina udhamini, fedha hizo zimesaidia matumizi kadhaa ikiwemo suala zima la
kusaka ubingwa msimu huu.
“Simba haina mfadhili wala mdhamini kwa sasa, hivyo fedha
zimesaidia kwenye mambo mengi ikiwemo kuhakikisha tunatwaa ubingwa safari hii,”
alisema.
Simba ilimweka Lyanga sokoni baada ya kocha Joseph Omog
kusema kuwa hakuwa kwenye mipango yake na kumtaka atafute timu nyingine ya
kuchezea ili kulinda kipaji chake hapo ndipo staa huyo akatimkia Fanja FC.
Lyanga alitua Simba akitokea DC Motema Pembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kusaini mkataba wa miaka miwili, lakini
akatumikia mwaka mmoja kabla ya kuuzwa Uarabuni.
Post a Comment