SIMBA msimu huu ilimsajili Laudit Mavugo kwa lengo la kuwa anaifungia mabao kibao timu hiyo, badala yake Shiza Kichuya ndiye anafunga sasa kocha wa timu hiyo, Joseph Omog amefunguka tatizo husika.
Kabla ya kutua Simba, Mavugo wakati anacheza Vital’O ya kwao Burundi alikuwa hatari kwa ufungaji lakini ameichezea Simba mechi saba na kufunga mabao matatu tu.
Sasa Omog raia wa Cameroon amesema Mavugo hakupata maandalizi ya kutosha ya kujiandaa na mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara kabla ya msimu kuanza pia utofauti wa ligi nao umempa changamoto.
 “Mavugo hakupata maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa ligi kuu ndiyo maana hafanyi vizuri, lakini kwa jinsi nilivyomwandalia mikakati ya umuweka sawa naamini atakuwa vizuri tu.
“Nawaomba wapenzi na mashabiki wa Simba waendelee kumuunga mkono kama ilivyokuwa hapo mwanzoni kwani muda si mrefu atakuwa vizuri,” alisema Omog.
Kwa upande wake Mavugo, alisema Ligi Kuu ya Burundi aliyocheza msimu uliopita ni tofauti na ya Tanzania kwani mabeki anaokutana nao hucheza kwa kukamia kupita kiasi na kumpa wakati mgumu.

Post a Comment

 
Top