KOCHA Mkuu wa Zesco United ya Zambia, George Lwandamina, anayewaniwa na Yanga amemsifia mshambuliaji wa timu hiyo, Obrey Chirwa, baada ya kusema ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu cha kucheza soka.
Chirwa alijiunga na Yanga msimu huu katika usajili wa dirisha dogo la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya timu hiyo kuingia hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini anaonekana kushindwa kuonyesha kiwango.
Lakini Lwandamina amesema anamfahamu vilivyo Chirwa na ni mmoja kati ya wachezaji wazuri wenye kipaji cha hali ya juu, tofauti na mashabiki wa Yanga wanavyomwona.
Chirwa ambaye alisajiliwa kwa dau nono, kwa sasa anaanzia benchi kutokana na kuonyesha kiwango duni katika mechi kadhaa alizocheza.
Akizungumzia mafanikio yake, Lwandamina alisema falsafa anayoitumia katika ufundishwaji ni kushambulia na kukaba ‘total football’.
Lwandamina alisema mfumo wake huo unamsaidia kuzifunga timu za ukanda wa Kaskazini mwa Afrika kama Zamalek ya Misri na nyinginezo.
“Niliweza kuwafunga Waarabu kwa sababu nilikuwa nasoma sana mifumo wanayotumia, lakini kuzifunga timu za ukanda wa Kaskazini unahitaji kuwa na wachezaji wa kujitoa kwa muda wote wa mchezo,” alisema Lwandamina.
Yanga wameanza kufanya mazungumzo na kocha huyo mwenye rekodi nzuri kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika, kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa Hans van der Pluijm.
Lwandamina aliiwezesha Zesco kuvuka hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, iliyokuwa kwenye Kundi A pamoja na Al Ahly ya Misri na Wydad Cassablanca ya Morocco.
Post a Comment