KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amewashukia wanaombeza kuwa hana msaada kwa bosi wake, Hans van der Pluijm akisema anamwachia Mungu kwa kila linaloendelea juu yake.
Kuna taarifa kuwa Yanga imepanga kulipangua benchi lote la ufundi baada ya kuelezwa kuwa katika mipango ya kumnasa kocha wa Zesco ya Zambia, George Lwandamina ili kumrithi Pluijm ambaye ataopewa jukumu la kuwa Mkurugenzi wa Ufundi Jangwani.
Sababu kubwa ya benchi la ufundi la Yanga kudaiwa kubadilishwa ni kutokana na kile kinachoelezwa kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yake, ikiwamo Mwambusi kumshauri bosi wake pale ilipohitajika kufanya hivyo.
Kutokana na kuona jinsi mashabiki wengi wa Yanga wanavyomnyooshea vidole, Mwambusi ameamua kufunguka akisema kuwa hana la kufanya zaidi ya kumwachia Mungu kwani ndiye muweza wa yote na kwamba kama riziki yake ipo Yanga, itaendelea kuwepo.
“Mimi sina neno najua upo kazini na unaandika kile unachokipata na kukisikia hiyo ni kazi yako lakini nakwambia jambo moja tu Mungu ndiye anapanga kila kitu hapa duniani kila jambo linategemea na Baraka zake,” alisema Mwambusi.
 Alisema anatambua  kuwa wapo watu ndani ya Yanga ambao wanatengeneza chuki baina yake na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pluijm ili waonekane hawafai na kuondolewa  katika kazi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo.
“Nafahamu kwamba kuna mambo yanatengenezwa hata mimi huu ugomvi wangu nilioambiwa  kwamba hatuelewani na mwenzangu (Pluiijm) ndio hao wanautengeneza sina cha kusema zaidi ya kumwachia Mungu kwa haya yote,” aliongeza Mwambusi.
Aidha Mwambusi alisema ni vyema kwa mtu yoyote anayetaka kurudi Yanga akasubiri mpaka Mungu mwenyewe atapoamua kuliko kusambaza taarifa za chuki na kugombanisha watu pasipo na ukweli wa aina yoyote.

Post a Comment

 
Top