STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe anaongoza kwa kutoa pasi za mwisho dhidi ya Shiza Kichuya ambaye wanafukuzana kwenye safu ya ufungaji bora msimu.
Kichuya yupo juu akiwa na mabao saba wakati Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa msimu uliopita akiweka kimiani mabao 21 mpaka sasa anayo sita.
Lakini kwa upande wa asisti Tambwe anaonekana kung’ara mpaka sasa kwani jumla ametoa tano katika mabao 24 waliyofunga Yanga mpaka sasa huku Kichuya akiwa nazo mbili katika mabao 21 ya Simba.
Kutokana na hali hiyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja akaona isiwe tabu, akasema kupungua kwa kasi ya ufungaji ya Kichuya kunatokana na timu hiyo kuwa na wafungaji wengi.
 “Watu wanatakiwa kuelewa kwamba Simba hii haimtegemei mtu mmoja katika kusaka ushindi, ukitaka kuamini hilo angalia katika mechi mbili zilizopita. Kichuya hajafunga lakini tumeshinda.
“Katika mechi hizo mbili ambazo Kichuya hajafunga, Mzamiru Yasin ndiye aliyefunga, hivyo kama tungekuwa tunamtegemea mtu mmoja sidhani kama tungekuwa hapa tulipo,” alisema Mayanja.
Mwenyewe Kichuya amewahi kuliambia gazeti hili kwamba: “Huwa siangalii nimefunga mabao mangapi, bali ninachoangalia ni kiasi gani nimeisaidia timu yangu kupata ushindi basi.
“Hilo ndilo jambo la kwanza kwangu, kisha mengine yanafuata ikiwemo ishu ya ufungaji bora.”

Post a Comment

 
Top