KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog ambaye
awali alikuwa akimuona straika Mrundi Amissi Tambwe kuwa ni mchezaji wa
kawaida, hatimaye sasa amekiri kuwa nyota huyo ni hatari katika kuzifumania
nyavu.
Hali hiyo imetokana na rekodi mpya ambayo Tambwe
ameibaini hivi karibuni ambayo pia amefanikiwa kuiandika ndani ya misimu mitatu
tangu atue hapa nchini akitokea Burundi.
Tambwe alisema: “Rekodi hiyo nilikuwa siijui
lakini hivi karibuni baada ya kukaa na kuanza kupitia daftari langu la
kumbukumbu, ndipo nikakumbana nayo, hakika nilijisikia vizuri sana.
“Namuomba Mungu anisaidie ili niweze kufanya
vizuri msimu huu nitakapokutana na Mbao FC pamoja na African Lyon niweze
kuzifunga ili rekodi yangu hiyo isiwe na shaka yoyote, kwani hizo ndiyo timu
pekee ambazo sijazifunga kwa sababu tangu nifike hapa nchini ndiyo zinashiriki
ligi kuu kwa mara ya kwanza,” alisema Tambwe ambaye tayari msimu huu
ameshazifumania nyavu mara nne katika mechi sita alizoitumikia Yanga mpaka
sasa.
Kwa upande wake Omog akimzungumzia mchezaji huyo
hivi karibuni, alisema: “Tambwe ni mchezaji ambaye anayajua majukumu yake ya
uwanjani na nimepata kusikia rekodi zake mbalimbali ikiwemo ya kuwa mfungaji
bora mara mbili pamoja na hii ambayo naisikia sasa ya kuzifunga timu zote za
ligi kuu ambazo amekutana nazo ndani ya misimu hiyo mitatu, nampongeza kwa hilo
kwani siyo kazi ndogo aliyoifanya.
“Hata hivyo, kuhusiana na bao alilotufunga hivi
karibuni, hilo siwezi kulizungumzia ila nachoweza kusema ni mchezaji mzuri,”
alisema Omog ambaye tayari ameshaiongoza Simba kucheza mechi saba bila ya
kufungwa huku ikiwa kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 17 pamoja
na mabao 13 ya kufunga.
Post a Comment