SHIZA Kichuya ana mabao matano katika Ligi Kuu Bara na klabu yake ya Simba, kama hujui ni kwamba kiungo huyo mshambuliaji anafanya kazi inayopaswa kufanywa na LauditMavugo na Ibrahim Ajibu.
Aliyepasua utendaji huo wa Kichuya ni kocha wake Joseph Omog anayekinoa kikosi cha Simba, kwani awali alikuwa amemuandaa winga huyo kuwa mtoa pasi za mwisho lakini amejiongeza kuwa mfungaji hatari.
Omog alisema wachezaji aliowaandaa na kuwategemea kwa ajili ya kufunga ni Ajibu, Mavugo pamoja na FredericBlagnon lakini bado hawajawa na kasi ya ufungaji kama Kichuya.
Alisema wakati anaandaa kikosi chake kwa ajili ya mechi za ligi kuu, alimuweka Kichuya kuwa mchezeshaji wa timu na mtengenezaji wa mabao kwa Ajibu, Mavugo na Blagnon lakini anashangaa sasa jamaa amekuwa mfungaji kuliko walengwa.
“Hata hivyo, nampongeza sana Kichuya kwani amekuwa msaada mkubwa sana kwetu kwa kutufungia mabao muhimu zaidi japokuwa yeye si mfungaji ninayemtegemea katika kikosi changu.
“Lakini kwa vile ameonyesha uwezo wa kufunga, hilo ni jambo zuri kwa timu na Ajibu, Mavugo na Blagnon nao wanatakiwa kufanya kama anavyofanya Kichuya,” alisema Omog,raia wa Cameroon.
Hadi sasa Simba imecheza mechi saba na ipo kileleni ikiwa na pointi 17 ikiwa na mabao 13 ambapo Ajibu amefunga mawili, Mavugo matatu na Blagnon moja tu.

Post a Comment

 
Top