WINGA wa Simba, Shiza Kichuya, amepania kuweka rekodi ya
kuwa mchezaji wa kwanza kufunga ‘hat-trick’ leo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC, utakaopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar
es Salaam.
Kichuya ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar,
ameibuka kuwa kipenzi cha mashabiki na viongozi wa Simba kutokana na kiwango
alichokionyesha hadi sasa akiwa na klabu hiyo ya Msimbazi.
Tangu aanze kuitumikia Simba katika mechi zake za VPL,
ameifungia timu hiyo mabao saba kati ya 17 ambayo wamefunga kwenye mechi nane
za msimu huu na kuongoza orodha ya wafungaji kwenye ligi kuu.
Mbali na kuongoza kwa kucheka na nyavu, Kichuya pia amepiga
pasi za mwisho tano ambapo ukijumlisha na mabao saba aliyofunga ina maana
amechangia kupatikana kwa mabao 12 kati ya 17 yaliyofungwa na Simba msimu huu.
Idadi hiyo ya Kichuya ya mabao ni sawa na asilimia 71 ya
mabao yote ya Simba waliyofunga msimu huu na hivyo kuonekana ni moja ya
wachezaji muhimu kwa miamba hiyo ya Msimbazi.
Kichuya alisema ana uhakika mkubwa wa kufunga ‘hat-trick’
leo kutokana na maandalizi mazito waliyoyafanya wachezaji wa timu hiyo na
benchi la ufundi linaloongozwa na Joseph Omog.
“Uwezo wa kufunga hat-trick leo ninao, si kwa sababu
tunacheza na timu dhaifu ndio nitambe hapana, huu ni mpango wangu ambao
nimeupanga na ninataka kuutimiza leo,” alisema Kichuya.
Simba inaingia uwanjani leo ikiwa imepania kuzidi kuongeza
pengo la pointi kati yake na wapinzani wao na ndiyo maana imepania kuibuka na
ushindi kwenye mechi yao ya leo dhidi ya Mbao FC.
Simba watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa
Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo kama Wekundu hao wa Msimbazi watashinda
watafikisha michezo 10 msimu huu bila kupoteza.
Kikosi hicho ambacho kipo chini ya kocha Mcameron, Joseph
Omog, kimeshinda mechi saba na kutoka sare mara mbili na hivyo kuongoza ligi
hiyo wakiwa na pointi 23 kibindoni.
Wekundu hao wa Msimbazi ambao msimu huu wamekuja na
kaulimbiu inayosema kila mchezo kwao ni fainali, itaingia uwanjani huku
ikihitaji pointi tatu muhimu kutoka kwa Mbao FC ili iweze kuendelea kujichimbia
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Simba wanaonyesha kuwa na uchu wa kupata ushindi katika kila
mechi ili kutimiza lengo lao la kutwaa ubingwa msimu huu, huku wakitoka kupata
ushindi wa mabao 2-0 kutoka kwa Kagera Sugar mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru,
Dar es Salaam.
Kwa upande wa Mbao FC iliyopanda daraja msimu huu, itaingia
kumkabili Mnyama huku ikiwa imetoka katika machungu ya kutandikwa 3-1 na Toto
Africans.
Katika msimamo wa ligi, Mbao FC inashika nafasi ya sita
ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi 10 ambayo iliweza kushinda mitatu,
sare mitatu huku ikiruhusu kufungwa michezo minne.
BINGWA
Post a Comment