KLABU ya Simba inaendelea kupata neema baada ya mwanachama wake, Mohammed Dewji ‘MO’ kumaliza tatizo la kuwalipa mishahara wachezaji ambao kwa sasa hawana tena presha na badala yake wanajua kila mwisho wa mwezi wanakwenda benki kuchota ‘mihela’ tu.
Kwa sasa klabu hiyo imekuwa ikiwalipa mishahara kwa wakati wachezaji hao, baada ya bilionea huyo ambaye ni mwanachama wao kuweka mzigo wa fedha ambazo zinaweza kuwasukuma mpaka Januari, mwakani.
Taarifa ambazo tumezipata kutoka Simba zinadai kuwa, Mo ameshaweka fedha benki ambazo ni mshahara wa wachezaji mpaka Januari mwakani, hivyo wachezaji hao hawatakiwi kuwa na presha yoyote juu ya mishahara yao.

Taarifa hizo zinadai kuwa, fedha hizo za mishahara ni moja ya ahadi yake kama mwanachama wa klabu hiyo wakati huu wakiwa kwenye mchakato wa kumkabidhi hisa asilimia 51.
“Ni kweli jamaa (MO) anajitolea sana kwa sasa, ameshatoa fungu la kutosha kwa ajili ya mishahara ya wachezaji, fedha hizo zitatosha mpaka Januari mwakani, hivyo kwa sasa hutasikia wachezaji wakilia njaa,” kilisema chanzo hicho.
Mbali na kutoa fedha hizo, pia inadaiwa kuwa, mfanyabiashara huyo ameagiza basi la kisasa ambalo litaingia muda wowote kwa ajili ya matumizi ya timu na hii yote ni kuifanya Simba kuwa ya kisasa zaidi.
Wekundu hao wa Msimbazi wapo kwenye mchakato wa kumpa Mo hisa asilimia 51 ili awekeze ambapo mwenyewe ameamua kujitolea mambo mengi, ikiwamo kutoa Sh milioni tano kila timu inaposhinda mchezo ili kuwapa motisha wachezaji, huku Sh milioni tano nyingine zikitoka kwa wadau mbalimbali wa kikosi hicho.


Post a Comment

 
Top