SIMBA kweli imedhamiria kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu hiyo ni baada ya kushinda mchezo 10 leo dhidi ya Mwadui ya Shinyanga.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Dimba la Kambarage mjini Shinyanga Simba ilipata ushindi wa mabao 3-0 na hivyo kuongeza ‘gepu’ dhidi ya watani wao Yanga ambao wao wana alama 24 na Simba wamefikisha 32.
Baada ya straika Laudit Mavugo kuonekana kutokuwa kwenye kiwango katika mchezo wa leo, Kocha Joseph Omog alimtoa dakika ya 42 na nafasi yake ilichukuliwa na Amme Ali.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Mohamed Ibrahim ambaye alipokea mpira kwa kifua akiwa ndani ya 18 kabla ya kupiga shuti ambalo kipa Shaban Kado alishindwa kulidaka.
Muuaji Shiza Kichuya kama kawaida yake naye alipiga bao maridadi akiunganisha krosi ya Mo Ibrahim muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Mo Ibrahim aliwainua tena mashabiki wa Simba kwa bao safi akiwa yeye na goli ambapo aliunganisha pasi murua kutoka kwa Ame Alli ambaye awali alifanyakazi ya ziada kuupata mpira huo kutoka kwa mchezaji wa Mwadui na kupiga krosi nzuri.

Wafungaji Ligi Kuu
Kichuya Simba 8
Mandawa Mtibwa 6
Tambwe Yanga 6
Mponda Ndanda 5
  

Post a Comment

 
Top