MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe, amesema mbio za
ufungaji bora kwenye Ligi Kuu Bara ni ngumu kutokana na ushindani uliopo lakini
ameahidi atapambana kuiwezesha Yanga kufanya kweli na ikibidi yeye kutetea tuzo
yake ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Mrundi huyo, ambaye kwenye mechi ya juzi ya ligi kuu dhudi
ya JKT Ruvu alifunga mabao mawili akitokea benchi, sasa amefikisha mabao sita
ikiwa ni moja nyuma ya Shiza Kichuya wa Simba anayeongoza akiwa na mabao
saba.
Kwa kasi hiyo na kwa tambo hizo ni wazi Tambwe amempa
angalizo Kichuya kuongeza bidii la sivyo atampita na yeye kushika usukani wa
kuongoza kwa mabao katika ligi hiyo.
Tambwe alisema haikuwa
kazi rahisi kufunga mabao mawili juzi kwa kuwa ametoka katika majeraha ya
kupasuka kwenye paji la uso katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na kusababisha ashonwe nyuzi sita.
"Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kufunga
mabao mawili, mabao hayo yametokana na juhudi na kujituma kwangu kwa
kushirikiana vema na wachezaji wenzangu ambao wamenitengenezea nafasi hizi za
kufunga.
"Nimefikisha mabao sita, lakini bado nina kibarua
kigumu cha kutetea kiatu changu cha dhahabu kutokana na ushindani mkubwa wa
ufungaji mabao, kama unavyoona wachezaji wanajitahidi kufunga mabao, najua
Kichuya ana saba ila mimi pia nitaendelea kujituma nifunge zaidi,” alisema
Tambwe.
Tambwe aliwahi kutwaa ufungaji bora katika ligi kuu msimu
wa 2013/2014 akifunga mabao 19 akiwa Simba, 2015/2016 akipachika 21 akiichezea
Yanga huku 2014/2015 akimaliza kwa kushika nafasi ya pili kwenye orodha ya
wafungaji akifumania nyavu mara 14.
Post a Comment