MWENDO wa dozi tu. Simba imeendelea kugawa dozi kwenye Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, baada ya kuizamisha Mbeya City kwa mabao 2-0 mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya  Sokoine jijini hapa.
Mabao ya Simba yalifungwa na Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya na kuifanya timu hiyo kuendelea kujikita kileleni ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza mechi nane.
Simba walianza kufanya shambulizi langoni mwa Mbeya City baada ya Fredrick Blagnon, kupoteza nafasi ya wazi ya kufunga ikiwa ni dakika ya kwanza.

Baadaye Simba walifanya shambulizi lingine baada ya Kichuya kuwatoka mabeki wa Mbeya City dakika ya nne, lakini alichezewa madhambi na mwamuzi wa mechi hiyo, Alex Mahagi, kuamuru upigwe mpira wa adhabu ambao haukuzaa matunda.
Simba walipata bao la kwanza dakika ya sita lililofungwa na Ajib, baada ya kupiga shuti kali la mpira wa adhabu nje ya eneo la 18  na kutinga moja kwa moja wavuni.
Kichuya naye aliendelea kung’ara kwa kucheka na nyavu karibu kila mechi baada ya kuipatia Simba bao pili dakika ya 34 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Jonas Mkude.
Mbeya City walifanya shambulizi na kupata kona, lakini kipa wa Simba, Vincent Angban alidaka kwa ufundi wa hali ya juu.
Hata hivyo, Blagnon alikosa penalti dakika ya 13 baada ya kuangushwa na mabeki wa Mbeya City katika eneo la hatari lakini mkwaju wake ulipanguliwa na kipa wa Mbeya City.
Katika dakika ya 63, Ame Ali wa Simba  aliingia kuchukua nafasi ya Blagnon ma kupoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya mabeki wa City kuokoa hatari iliyokuwa inakwenda langoni mwao.

Post a Comment

 
Top