KOCHA Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja,
amesema wapinzani wao Yanga wamechoka na hata kocha wao Hans van Der Pluijm
analijua hilo.
Kocha huyo ameweka wazi suala hilo wakati Simba
wakiwa juu ya timu zote katika msimamo wa Ligi Kuu Bara wakijikusanyia pointi
17 kwenye mechi zao saba ambapo wapo mbele ya Yanga kwa pointi sita, ingawa Jangwani
wana mchezo mmoja mkononi.
Mayanja aliyewahi kucheza soka Klabu ya Esperance
ya Tunisia, amesema, Pluijm anatambua kuwa morali ya wachezaji wake kwa sasa
imeshuka kwa sababu ya uchovu miongoni mwa mastaa wake ambapo jambo hilo ni
faida kwao na watalichukulia kama sehemu ya kutwaa ubingwa.
“Unajua Yanga wamecheza mechi nyingi bila ya
kupumzika ukianza kwenye Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho na sasa ligi kuu
ambapo wachezaji wake wa kikosi cha kwanza karibia wote wamechoka na hilo kocha
wao Pluijm analijua lakini amekuwa mbishi na anaendelea kuwatumia hivyohivyo,
jambo ambalo linawasababisha kuchoka zaidi lakini ni faida kwetu katika
harakati za kutwaa ubingwa kwa sababu wao kwenye michezo yao mingi wanapata
matokeo mabaya.
“Mtazame kama Ngoma (Donald) kiwango chake
hakiendani kabisa na msimu uliopita ambapo ameshindwa kufunga katika mechi
zaidi ya tatu ukiondoa ile na Mwadui lakini sisi tunafurahia kuona wao wanazidi
kuboronga kwa sababu inakuwa nafuu kwetu ya kutwaa ubingwa kutokana na mpinzani
mkuu ndiyo hivyo anapotea,” alisema Mayanja.
Post a Comment