WAKATI Yanga
wakicheza leo dhidi ya Kagera Sugar, kocha mkuu wa kikosi hicho, Hans van Der Pluijm,
kiroho kinamdunda kwani anaweza akatumbuliwa ndani ya saa 48 kuanzia sasa.
Unajua
ikoje! Tayari kuna mipango ya chini kwa chini ya kumleta kocha mpya kutoka
Zesco ya Zambia, George Lwandamina, ambapo ni kama Pluijm anatafutiwa sababu
apigwe chini.
Kama Yanga
watapata matokeo mabaya katika mchezo wa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba, mkoani
Kagera, hiyo inaweza kuwa fimbo ya kumchapia Pluijm.
Licha ya
ukweli kwamba kuna idadi kubwa ya wanachama na mashabiki wanaomkubali Pluijm
kutokana na kazi kubwa aliyoifanya hasa msimu uliopita, lakini imeonekana
baadhi ya watu wa timu hiyo wamechochwa na Mholanzi huyo.
Taarifa za
uhakika ambazo tumezipata zinadai kuwa mazungumzo kati ya Yanga na kocha huyo
mpya kutoka Zambia, yanaelekea pazuri hali ambayo inadhihirisha kuwa muda
wowote Pluijm anaweza akaambiwa afungashe kila kilichochake.
Wanaotaka
Pluijm aondoke wanadai kuwa Mholanzi huyo ni kama ameishiwa mbinu na sasa
wanataka kocha mwingine ambaye atakuja na kitu kipya ambapo kura imemwangukia
Lwandamina.
Pia taarifa
hizo zinadai kuwa Pluijm aliambiwa aifikishe Yanga mbali katika michuano ya
kimataifa, lakini wakatolewa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika
jambo ambalo ni kinyume na makubaliano ya pande hizo mbili.
Taarifa
kutoka Yanga zinadai kuwa Pluijm ataondoka na benchi lake zima akiwamo kocha
msaidizi, Juma Mwambusi pamoja na Meneja wa kikosi hicho, Hafidh Saleh, ili
kumpa nafasi huyo anayekuja aje na kikosi kazi kipya.
Wanaotajwa
kuingia na kocha huyo mpya ni kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Boniface
Mkwassa, ambaye anaweza kuwa kocha msaidizi, huku Salvatory Edward akipigiwa
chapuo kuwa meneja wa timu.
Katika
mchezo wa leo, Pluijm anatakiwa kuzichanga vizuri karata zake ili kushinda na
kuondoka na pointi zote tatu dhidi ya Wakata Miwa hao ambao nao wamepania
kuutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani.
Msimu
uliopita timu hizi zilipokutana Yanga waliibuka kidedea baada ya kushinda
michezo yote miwili wakianza kushinda mabao 2-0, mchezo wa mzunguko wa kwanza
Kagera wakiwa wenyeji Uwanja wa Kambarage na Wanajangwani hao wakashinda tena
mabao 3-1 mzunguko wa pili Uwanja wa Taifa.
Katika
mchezo wa leo, Yanga itawategemea zaidi washambuliaji wake, Donald Ngoma pamoja
na Obrey Chirwa ambaye ameanza kuonyesha cheche zake tofauti na alivyoanza.
Hata hivyo,
Yanga hawatakiwi kuwadharau wapinzani wao hao kwani msimu huu wanaonekana
kujipanga vizuri chini ya kocha wao, Mecky Mexime, ambaye walimchukua kutoka
Mtibwa Sugar.
BINGWA
Post a Comment