DUH! Licha ya kwamba mshambuliaji wa Simba,
Mrundi, Laudit Mavugo hakufunga bao walipoumana na Yanga wiki iliyopita, lakini
amesema si timu ya kutisha sana, anaiona ya kawaida na zaidi walikuwa na bahati
wamenusurika kuchezea kichapo licha ya wao kuwa pungufu.
Mavugo amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa
mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar na kuisha kwa sare ya 1-1 ambapo
alikiri kuwa Yanga ni timu kubwa lakini haitishi kama inavyoelezwa zaidi ya kutegemea
uwezo wa mchezaji mmojammoja.
“Sikatai Yanga ni timu kubwa, nilikuwa nikisikia
Yanga ni wazuri sana, leo (juzi) nimekutana nao, si wabaya lakini zaidi ni
uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kwa jinsi nilivyowaona leo (juzi) na kama
tungekuwa tumetimia, Mkude (Jonas) asingepewa nyekundu, tungewafunga bila
tatizo.
“Muda mwingi tuliwazidi, ukiangalia kipindi cha
pili chote tulicheza pungufu lakini tulicheza vizuri zaidi yao na tukafunga bao
tukiwa wachache. Kuhusu kutofunga leo, huwa inatokea na mechi yenyewe, muda
mwingine unaweza kupanga hivi na ikawa tofauti,” alisema Mavugo aliyefunga
mabao matatu mpaka sasa.
Katika mchezo huo, Mavugo aliyewahi kuichezea
Vital’O ya Burundi, alipata nafasi ya kupiga mashuti matatu katika lango la
Yanga, yote hayakuwa na madhara na yalipita nje ya lango.
Post a Comment