WAKATI baadhi ya mashabiki wa Simba
wakiendelea kulalamikia bao la Amis Tambwe kwamba alifunga baada ya kugusa
mpira kwa mkono, mwenyewe amewaambia waende uwanjani leo wakashuhudie uwezo
wake.
Tambwe, ambaye ni mfungaji bora wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, baada ya kutia kimiani mabao 21,
alifunga bao hilo katika mchezo wao dhidi ya Simba, uliochezwa katika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, Oktoba Mosi mwaka huu, huku mchezo huo ukimalizika kwa
sare ya 1-1.
Tambwe alisema yupo kwa ajili ya
kuisaidia Yanga na atafunga kila anapopata nafasi, hivyo mashabiki wajitokeze
uwanjani waone atakavyoweza kuifunga Mtibwa.
“Ah Ah eti bao la mkono, hakuna kitu
kama hicho, waje na kesho (leo) waone mabao mengine, kwani nitafunga kila
ninapopata nafasi ya kufanya hivyo, kikubwa Yanga ipate ushindi,” alisema.
Kwa sasa Tambwe ameshaifungia Yanga
mabao manne katika michezo sita iliyocheza, akiwa nyuma ya Shiza Kichuya wa
Simba, aliyetupia mabao matano kwenye mechi saba alizochezea timu yake.
Post a Comment