LICHA
ya mara kwa mara Ally Mustapha ‘Barthez’ kuonekana kutokuwa makini awapo
langoni, lakini hilo lisikufanye uamini kwamba hafai kwani takwimu zinaonyesha
yeye na mwenzake, Deogratius Munishi ‘Dida’ wamecheza mechi sawa kwenye kikosi
chao cha Yanga huku kila mmoja akilinda vilivyo lango lake.
Barthez
na Dida kila mmoja msimu huu amecheza mechi tano za ligi ndani ya kikosi hicho
katika mechi kumi za Yanga na kufanikiwa kuifikisha timu yao nafasi ya pili kwa
kujikusanyia pointi 21.
Barthez
ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya kidole aliyoyapata kwenye mchezo wao dhidi
ya Simba, Oktoba Mosi, mwaka huu walipotoka sare ya bao 1-1, katika mechi zake
tano hakuruhusu bao (clean sheet) mara tatu, sawa na Dida, lakini tofauti yao
ni kwamba Barthez ameishuhudia Yanga ikifungwa mchezo mmoja, huku Dida akiwa
bado hajapoteza mechi hata moja.
Dida
alianza kudaka msimu huu ambapo mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya African Lyon
ambapo Yanga ilishinda 3-0 kwa mabao ya Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma
Mahadhi.
Baada ya mechi hiyo, Dida
hakuonekana tena langoni kutokana na kukumbwa na msiba wa baba yake, nafasi
yake aliichukua Barthez, lakini Dida alikuja kuonekana tena kwenye mchezo wa
saba dhidi ya Mtibwa ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1. Wafungaji wakiwa ni
Obrey Chirwa, Msuva na Donald Ngoma, huku Mtibwa bao lao likifungwa na Haruna
Chanongo.
Kuanzia hapo mpaka juzi
Jumamosi, Dida amekuwa akikaa langoni ambapo kwenye mechi hizo, matokeo
yalikuwa hivi; Azam FC 0-0 Yanga,
Toto African 0-2 Yanga na Kagera Sugar 2-6 Yanga.
Kwa upande wa Barthez,
mechi zake tano zilikuwa hivi; Ndanda 0-0 Yanga, Yanga 3-0 Majimaji, Mwadui 0-2
Yanga, Stand United 1-0 Yanga na Yanga 1-1 Simba.
Post a Comment