KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon,
Joseph Omog, amemtahadharisha kiungo wake mshambuliaji, Shiza Kichuya,
akimwambia hatakiwi kubweteka na sifa anazoendelea kuzipata na badala yake
aongeze bidii ndani ya uwanja.
Kichuya ambaye ni mchezaji tegemeo
kwenye timu hiyo, ameshaifungia Simba mabao matano na ndiye anayeongoza kwenye
chati ya ufungaji kwenye Ligi Kuu Bara huku akikumbukwa kwa kuipa timu yake
pointi tatu dhidi ya Azam FC na pointi moja kwa bao maridadi la dakika ya 87
dhidi ya Yanga.
Kiungo huyo mwenye kasi kubwa ndani
ya uwanja, alijiunga na Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Mtibwa Sugar
kwa dau la Sh milioni 30.
Omog alisema hampangi mchezaji
katika kikosi chake kutokana na umaarufu huku akitaja juhudi binafsi ndani ya
uwanja na kujituma kuwa ndiyo kigezo anachokitumia katika kupanga timu.
Omog alisema, anafurahishwa na
kiwango kikubwa kinachoonyeshwa na Kichuya uwanjani ambacho kimemfanya
kuonekana bora na tegemeo kwenye timu kubwa kama Simba.
Aliongeza kuwa, kikubwa
anachotakiwa kufanya kiungo huyo, ni kuendelea kulinda kiwango chake ili
kisishuke kwa kutimiza majukumu yote atakayopewa katika timu.
"Wachezaji wengi wanafeli
katika kupata mafanikio kutokana na kuridhika, pia kubweteka baada ya kulewa sifa
pale wanapofanya kitu kizuri na kusifiwa.
"Hali hiyo, sitaki imtokee
Kichuya baada ya kuifungia timu yake bao la kusawazisha katika dakika ya 87
kwenye 'derby' na Yanga iliyochezwa hivi karibuni.
"Kikubwa anachotakiwa kufanya hivi
sasa ni kuendelea kulinda kiwango chake ili kisishuke kwa kutimiza majukumu
yote atakayopewa katika timu ikiwemo kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga
mabao," alisema Omog.
Post a Comment