Mayanja: Simba hatumtegemei mtu
KOCHA msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amedai kuwa klabu hiyo ni zaidi ya mtu mmoja na ndiyo maana benchi la ufundi limepania kuhakikisha miamba hiyo ya Msimbazi inafanya makubwa bila kumtegemea mchezaji mmoja bali wote waliopo kikosini.
Mayanja aliyasema hayo juzi baada ya kumalizika mchezo kati ya Mbeya City na timu yake ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, wafungaji wakiwa Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya.
Kauli hiyo ilikuja baada ya kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya Msimbazi kuanza bila mastaa wake wa kimataifa, Laudit Mavugo na Juuko Murshid katika mchezo huo muhimu wa ugenini.
Akilizungumzia hilo, Mayanja alisema Simba ya mwaka huu haimtegemei mchezaji mmoja kwa sababu imefanya usajili mzuri na kila mchezaji ana uwezo wa kuibeba timu.
“Suala la kutegemea mchezaji mmoja au wachezaji wachache limepitwa na wakati, Simba hii inategemea wachezaji wote na kila mmoja atatumika pale inapobidi,” alisema Mayanja.
Akimzungumzia Murshid ambaye analalamikiwa ni mchezaji mzuri lakini anawekwa benchi, Mayanja alisema lazima watu wajue kuwa uchezaji wa timu ya taifa na klabu una tofauti.
“Juuko ni mchezaji mzuri, ana nafasi ila tulimpumzisha baada ya kutoka kwenye majukumu ya kitaifa na hakuwa amefanya mazoezi na wenzake,” alifafanua Mayanja.
Kuhusu mikakati ya michezo ya ugenini Mayanja alisema: “Tumeanza na ushindi Mbeya haikua kazi rahisi, lakini mipango ya mechi hii ilikua ni kucheza kwa kasi bila woga kama tupo nyumbani ili tupate ushindi, hili limetusaidia na tutafanya hivyo kwenye mechi zijazo pia.”
Simba hadi sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza michezo nane ikishinda sita na kutoka sare miwili ikiwa haijapoteza mechi hata moja msimu huu.
Katika hatua nyingine mchezo wa juzi kati ya Simba na Mbeya City uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa, uliingiza kiasi cha shilingi milioni 60 hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Chama cha Soka Mbeya, Haroub Selemani, aliyedai kuwa mapato hayo ni ya rekodi.
Post a Comment