SIKU chache
baada ya Yanga kuachana na kocha Hans van Pluijm, wachambuzi wa soka wamehofia
uwezekano wa timu hiyo kutetea ubingwa wake msimu huu.
Yanga ambao
ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mpaka sasa wanashika nafasi ya
pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwaacha mahasimu wao Simba
kushika usukani kwa tofauti ya pointi tano.
Simba
inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza michezo 11
huku mabingwa hao watetezi wakiwa na pointi 24 baada ya kushinda mchezo wa jana
dhidi ya JKT Ruvu.
Wachambuzi
mbalimbali wakiongozwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Ali Mayay, alisema klabu
hiyo ya Jangwani msimu huu kuna uwezekano mdogo wa kutetea ubingwa kutokana na
mambo jinsi yanavyokwenda ndani ya timu hiyo.
Alisema siku
zote haishauriwi klabu kufanya mabadiliko ya kocha katikati ya msimu labda
ikitokea dharura kubwa.
“Kila kocha
huja na falsafa zake ndio sababu kubwa ambayo inashauriwa kubadilisha benchi la
ufundi msimu unapomalizika hivyo ubingwa wa Yanga msimu huu ni bahati nasibu,”
alisema.
Alisema
Yanga wana kazi ngumu ya kutetea ubingwa huo huku wakiwa na upinzani mkubwa
kutoka kwa watani zao wa jadi, Simba ambao hawajatetereka mpaka sasa.
“Kama kocha
George Lwandamina anakuja na falsafa kama za Pluijm basi Yanga itaendelea
kufanya vema, lakini kama anakuja na falsafa zake kama alivyofanya kocha wa
Azam watafeli na wasitarajie kutetea ubingwa,” alisema.
Naye Kennedy
Mwaisabula ‘Mzazi’, alisema Yanga kwa sasa ipo vizuri lakini mabadiliko hayo ya
benchi la ufundi yanaweza kuwaathiri hasa kushuka kiwango.
“Yanga mpaka
sasa wamecheza mechi 10 (kabla ya mchezo wa jana), lakini bado wana mechi 20
mkononi pamoja na mzunguko wa pili na wapo vizuri lakini mabadiliko haya
yanaweza kuwavuruga na kupoteza mwelekeo,” alisema.
Alisema
mabadiliko hayo yanaipa ugumu Yanga kutetea nafasi yao ya ubingwa walioupata
mwaka jana hivyo wanapaswa kuwa makini kwa kipindi hiki.
“Mabadiliko
yataigharimu timu sana, kwa sasa inafanya vema ila inaweza kupunguza morali
yake, kwangu mimi sikuona tija kwa kipindi hiki wangesubiri msimu ujao,”
alisema.
Post a Comment