HAKUNA kung’ata maneno aisee! Beki wa zamani wa Yanga, Godfrey Taita, alikuwa na kazi pevu ya kuwazuia Simba katikati ya wiki iliyopita alipokuwa akiitetea timu yake ya Kagera Sugar na baada ya mchezo huo kumalizika, alishindwa kujizuia na kutamka wazi kuwa ubingwa unawahusu Wekundu hao wa Msimbazi.
Beki huyo wa zamani wa Yanga, licha ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo huo, alijikuta timu yake ikimaliza dakika 90 ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Taita ni mmoja wa mabeki tegemeo katika kikosi cha Kagera Sugar, ambapo Wakata Miwa hao ni moja ya timu zilizoruhusu mabao machache kutokana na uimara wa safu yao ya ulinzi.
Taita alisema, Simba ya msimu huu iko vizuri sana, ina muunganiko mkubwa tofauti na misimu mitatu ya nyuma ambapo ilikuwa inamtegemea mchezaji mmoja kuamua matokeo.
TAITA
“Kwa sasa wanacheza vizuri, tofauti na misimu ya hivi karibuni, angalia hata katika mchezo wetu huu jinsi walivyocheza kwa uangalifu wa hali ya juu kuhakikisha hawaruhusu bao, huku wao wakilazimisha kufunga.
“Naamini kama wataendelea na kasi hii, bila shaka wanaweza wakatwaa ubingwa wa msimu huu, licha ya kwamba Ligi bado ni mbichi na timu nyingine zinaendelea kujipanga,” alisema.
DIMBA

Post a Comment

 
Top