MIKAKATI ya klabu ya Simba kuelekea kwenye mechi zake za mkoani Mbeya si ya mchezo, huku timu hiyo ikiwa imepania kuhakikisha hakuna atakayepona katika mechi zao hizo za ugenini.
Simba ambayo kwa sasa imeweka pembeni matokeo ya bao 1-1 iliyoyapata mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Yanga, inatarajiwa kutoka nje ya Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Meneja wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, alisema kwa sasa kikosi hicho kinahamisha nguvu zake kwenye michezo yake ya mikoani ili kuendelea kuweka rekodi ya kutofungwa.
Alisema kikosi hicho kilichokuwa na programu maalumu kwenye Uwanja wa Kinesi, kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam Jumamosi.
“Timu inaondoka Jumamosi kwa ajili ya mchezo wetu wa Oktoba 12 mkoani Mbeya, hivyo yale yaliyotokea yote tumeshayasahau, kwa sasa tunataka kuendeleza rekodi hiyo ya kutofungwa katika michezo ya mikoani licha ya changamoto zilizopo katika viwanja vingi, lakini tutapambana,” alisema.

“Moto huu tulioanza nao tunataka uendelee na hilo linawezekana kwa sababu tuna kikosi kinachoweza kuibuka na ushindi katika mazingira yoyote yale, pia morali yetu inaongezwa kwa sababu tunataka kuchukua ubingwa kwa msimu huu,” alisema.
Mgosi aliendelea kusema kuwa kikosi hicho ambacho kilipata ziara ya mkoani Iringa, safari hiyo imekufa na sasa kinaendelea na mazoezi kama kawaida kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi.
“Safari ya Iringa imekufa kwa hiyo kwa sasa sisi tunajiandaa na mikakati kabambe ya kuhakikisha tunaibuka na ushindi, hatutaki sare tena zinatosha tulizozipata,” alisema.
Katika hatua nyingine, kikosi hicho pia kimeanza mikakati ya nje ya uwanja, ikiwa sambamba na wachezaji kupewa bonas kutoka kwa mfadhili wao, Mohammed Dewji.
“Timu imejipanga sawasawa ikiwa sambamba na kukwepa hujuma, ambapo tayari wametanguliza baadhi ya watu mkoani Mbeya, huku tayari Mo ameshatoa bonas ya Sh milioni 10,” alisema.

Katika hatua nyingine, Nahodha wa Simba, Jonas Mkude, alisema kasi walioionyesha katika michezo yao dhidi ya Yanga ndio watakayoingia nayo kwenye mechi za mikoani.
“Mipango yetu ni kuona tunashinda nyumbani na ugenini, kwa mechi zetu zote tulizocheza Dar  tumefanikiwa kuzitendea haki, hivyo majeshi yetu yanahamia mikoani,” alisema Mkude.

Post a Comment

 
Top