KOCHA Hans Pluijm ambaye mwanzoni mwa wiki hii alitangaza kujiuzulu kuinoa Yanga, amefunguka kuwa, inamuuma kuondoka ndani ya klabu hiyo, huku akisema popote aendapo ataikumbuka timu hiyo na mashabiki wake.

Pluijm ambaye alifikia uamuzi wa kuandika barua ya kujiuzulu baada ya Yanga kudaiwa kumleta nchini Mzambia, George Lwandamina kuchukua nafasi yake huku yeye akiwa bado kikosini, amesema hana ugomvi na mtu na anaondoka kwa amani kwani miaka yote aliyokaa klabuni hapo alikuwa na ushirikiano na kila mtu.

Kocha huyo aliyeiongoza Yanga kuchukua mataji matatu msimu uliopita, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA pamoja na kuifikisha Yanga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika, amesema licha ya kuondoka, lakini viongozi wa Yanga walichokifanya ni kumkosea, hivyo hana budi kuachana nayo.


“Nitaimisi sana Yanga pamoja na mashabiki wake wote kwa ujumla, nawakubali kutokana na yale mazuri waliyonifanyia.

“Walichonifanyia viongozi si kitu kizuri, kwa sababu walikuwa na mazungumzo na kocha mwingine bila ya kunitaarifu chochote, walipaswa kuniambia kabla ili tuweze kujadiliana itakavyokuwa, lakini hawakufanya hivyo,” alisema Pluijm.

Post a Comment

 
Top