LICHA ya kuondoka kwa Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans van der Pluijm, kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, kimeonyesha hakuna matatizo hasa baada ya jana kuendeleza dozi nene kwenye mchezo wa ligi hiyo.

Yanga ambayo jana iliongozwa na kocha msaidizi, Juma Mwambusi, iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Alikuwa ni mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa ambaye hivi sasa ameendelea kutakata na kuwa ‘mtamu kama mcharo’ kwa kufunga kila mechi ambaye alianza kuwainua mashabiki wa Yanga vitini kwa kufunga bao la kuongoza katika dakika ya tano tu ya mchezo huo.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 24 wakishika nafasi ya pili huku Simba wakiwa kileleni kwa pointi 29 kutokana na kucheza mechi 11 kila mmoja.
 Chirwa alimalizia pasi safi ya Simon Msuva aliyewahi mpira uliotulizwa vibaya na beki wa JKT Ruvu kabla ya kutoa pasi safi iliyomkuta mfungaji katika nafasi nzuri naye hakufanya ajizi.

JKT Ruvu almanusura wapate bao dakika ya tisa baada ya mshambuliaji wao, Pera Mavuo, kushindwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Atupele Green na shuti la Mavuo lilitoka nje.
 
Donald Ngoma alimtengea Chirwa pasi nzuri dakika ya 11, lakini shuti lake lilidakwa na kipa wa JKT Ruvu, Said Kipao. Yanga walipoteza nafasi nyingine dakika ya 18 baada ya Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kupiga shuti kali na kugonga mwamba.

JKT Ruvu walifanya shambulizi zuri dakika ya 22 baada ya Green  kumpenyezea pasi Hassan Dilunga, lakini shuti lake lilitoka nje.

Hata hivyo, Yanga walipoteza umakini baada ya Kessy kufanya kazi nzuri dakika ya 34, lakini Chirwa alishindwa kufunga tena baada ya kipa wa JKT, Kipao kuondoa hatari hiyo.

Yanga walizidi kulisakama lango la JKT Ruvu ambapo Msuva alishindwa kumalizia pasi ya mwisho ya Deus Kaseke, baada ya shuti lake kutoka nje.

Tambwe aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Ngoma katika kipindi cha pili,  aliipatia Yanga bao la pili dakika ya 56 akiyatumia makosa ya beki wa JKT  Ruvu kushindwa kumdhibiti mapema na kuachia shuti lililojaa wavuni moja kwa moja.

Yanga walipata bao la tatu dakika ya 83 kupitia kwa Msuva baada ya kumtungua kipa ambaye alikuwa ameliacha lango lake.

Tambwe alifunga bao la nne dakika za lala salama, baada ya kutumia makosa ya beki wa JKT na kipa wao kutegeana kuokoa mpira, kisha Tambwe kuwazidi ujanja na kuugusa mpira ambao uliwapita wote wawili na kutinga kimiani.

Tambwe jana alifunga bao lake la 60 katika Ligi Kuu Tanzania Bara katika misimu mitatu ambapo alifunga mabao 19 akiwa na Simba katika msimu wa kwanza, akafunga mabao 14 katika msimu wa pili ambapo aliifungia Yanga mabao 13 na moja alifunga akiwa Simba, msimu uliomalizika alifunga mabao 21 na sasa ana mabao sita.

Ushindi wa jana umeifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga kuendelea kupaa, kwani imefunga mabao 10 katika mechi mbili jambo ambalo halijawahi kufanywa na safu nyingine ya ushambuliaji katika msimu huu wa ligi kuu.





Post a Comment

 
Top