KOCHA George
Lwandamina, ambaye muda wowote atatua nchini kuinoa Yanga, amesema yupo tayari
kufanya kazi na kocha wa sasa, Hans van der Pluijm, ambaye anatazamiwa kupewa
cheo cha Mkurugenzi wa Ufundi.
Yanga
wamefanya mazungumzo ya chini kwa chini na kocha huyo ambaye anaifundisha Zesco
ya Zambia, ambapo wiki iliyopita alikuja nchini na taarifa zinadai kuwa
alikutana na viongozi wa Wanajangwani hao na kufanya makubaliano ya awali.
Taarifa hizo
ambazo hazina shaka, zinadai kuwa Yanga wamekubaliana na kocha huyo kumpa
mkataba wa miaka miwili, licha ya kwamba pande zote mbili zimekuwa zikishindwa
kuweka wazi jambo hilo.
Baada ya
taarifa hizo kuvuja na kumfikia kocha wa sasa, Pluijm, Mholanzi huyo aliamua kuandika
barua ya kujiuzulu, mpaka pale zilipofanyika juhudi za kumrudisha tena ambapo
alikubali na leo atakuwa kwenye benchi wakati kikosi hicho kitakapowakabili
Mbao FC Uwanja wa Uhuru.
Mmoja wa
watu wa karibu wa Lwandamina ameliambia DIMBA kuwa, kocha huyo amesema hana
tatizo lolote na anaweza kufanya kazi kwa ukaribu na Pluijm, lengo likiwa
kuipatia Yanga mafanikio.
“Mwenyewe
(Lwandamina) wala hana tatizo, yupo tayari kufanya kazi na Pluijm, kwani
anatambua kuwa kocha huyo anao uwezo mkubwa sana na anayajua vizuri mazingira
ya Tanzania.
“Yeye
anaamini kwamba, akiwa kama kocha mkuu na Pluijm akawa mkurugenzi wa ufundi,
wanaweza wakaifanya Yanga kuwa ya kimataifa zaidi na ndiyo maana hasiti kufanya
kazi na mwenzake huyo,” kilisema chanzo hicho kutoka Zambia.
Taarifa
zaidi zinadai kuwa, Lwandamina ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha soka,
atatua jijini Dar es Salaam muda wowote kuanza kibarua chake na viongozi wa
Yanga wanataka kukaa meza moja na Pluijm kumshawishi akubali cheo kipya cha
ukurugenzi wa ufundi.
Post a Comment