WINGA teleza wa Simba, Shiza Kichuya, amezua mjadala mzito kwa mashabiki wa timu hiyo na wengineo nchi nzima, akifananishwa uchezaji na uwezo wake kwa ujumla na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Ubelgiji, Mbwana Samatta.
Samatta alitokea katika kikosi cha Simba na kutua TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako aling’ara, ikiwamo kuibuka kuwa mfungaji bora Afrika na mwisho wa siku, kutua Genk ya Ubelgiji.
Pamoja na Tanzania kuwapo na wachezaji kadhaa wenye uwezo wa hali ya juu, lakini wapenzi wa soka nchini wamekuwa wakikosa wa kumlinganisha na Samatta.
Lakini baada ya Kichuya kutua Simba na kuanza msimu wake wa kwanza Msimbazi kwa kishindo, akiwa amefunga mabao yake sita hadi sasa, tayari ameanza kutabiriwa makubwa akitajwa huenda akafuata nyayo za Samatta.
Kati ya mambo yanayowafanya wapenzi wa soka kumfananisha Kichuya na Samatta, ni uwezo wake wa kumiliki mpira, kasi, ujanja na mbinu za kuwatoka mabeki na kufunga mabao.
Blog hii ilimtafuta Kichuya kueleza juu ya maoni ya mashabiki hao ya kumfananisha na Samatta alisema yeye binafsi haoni tatizo la kufananishwa na mshambuliaji huyo wa Genk na kusisitiza atafanya kila awezalo kumpiku Samatta.
“Sina tatizo kufananishwa na Samatta hii inatokana na mafanikio aliyoyapata yeye  na mimi yananiumiza sana kichwa na Mungu akijaalia nataka nifike mbali zaidi ya alipofika Samatta,”alisema Kichuya.
Alisema haiwezekani nchi yenye idadi zaidi ya watu milioni 40 kutoa mtu mmoja anayecheza soka la kulipwa katika bara la Ulaya na kuahidi kufanya makubwa zaidi msimu huu.
“Kwanza ili ndoto yangu itimie lazima niondoke hapa kwenda nje na sio kwenda Yanga nasema Simba ndio timu yangu ya mwisho kuichezea hapa Tanzania, napambana msimu huu tupate tiketi ya kucheza michunao ya kimaifa niweze kuonekana kupitia michuano hiyo, ” aliongeza Kichuya.
CHANZO: BINGWA

Post a Comment

 
Top