Tujikumbushe ushindi wa Yanga hatua kwa hatua
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana walionekana kurejesha makali yao baada ya kuiadhibu Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyosuasua katika mechi mbili zilizopita baada ya kufungwa na Stand United na kutoka sare na mahasimu wao jadi, Simba walianza mchezo huo kwa kasi ambapo dakika ya kwanza, Juma Abdul, alipiga krosi lakini ilitoka nje huku dakika ya nne ikifanya shambulizi lingine ambapo Obrey Chirwa, aliamba ambaa na mpira na kupiga shuti lililoishia mikononi mwa kipa wa Mtibwa Sugar, Benedict Tinoco.
Wakicheza kwa kujiamini zaidi, Yanga waliendelea kulisakama lango la Mtibwa na dakika ya 18, Chirwa alifanya kazi nzuri ya kuukokota mpira kuanzia katikati mwa uwanja lakini beki, Dickson Daud aliutoa na kuwa kona.
Dakika ya 29, Yanga walifanya shambulizi lingine kali ambapo Thaban Kamusoko, aliachia shuti kali ambalo lilidakwa kwa ustadi na kipa wa Mtibwa Sugar.
Mtibwa Sugar walijibu shambulizi dakika ya 33 ambapo Haruna Chanongo, alikimbia na mpira akitokea winga ya kushoto lakini shuti lake lilishindwa kulenga lango.
Yanga ilijipatia bao dakika ya 44 likifungwa na Chirwa baada ya kupokea krosi kutoka kwa Simon Msuva kutoka winga ya kulia likiwa ni bao lake la kwanza tangu asajiliwe na klabu hiyo akitokea FC Platinums ya Zimbabwe.
Bao hilo lilimfanya Chirwa ambaye ni mchezaji ghali kwenye ligi hiyo kutoa gundu kama ilivyokuwa kwa mchezaji wa Manchester United, Paul Pogba ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya dunia ya kununuliwa kwa fedha nyingi.
Kipindi cha pili Yanga walimtoa Deus Kaseke na nafasi yake kuchukuliwa na Geofrey Mwashiuya. Dakika ya 47, Chirwa alikokota mpira akitokea winga ya kushoto na kuachia shuti kali ambalo lilitoka nje ya lango.
Dakika ya 52, Tambwe alishindwa kuunganisha krosi ya Mwashiuya baada ya kurusha mguu uliopishana na mpira. Katika kipindi hicho cha pili ambapo timu zote zilifunguka na kucheza soka safi, Mtibwa Sugar ilipata bao la kusawazisha dakika ya 63 likifungwa na Chanongo, baada ya mabeki wa Yanga kufanya uzembe kuokoa hatari langoni mwao.
Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya Yanga kuongeza mashambulizi langoni mwa Mtibwa na kufanikiwa kuandika bao la pili dakika ya 73 likifungwa na Msuva.
Yanga ilifanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Chirwa na Said Juma Makapu na nafasi zao kuchukuliwa na Donald Ngoma na Mbuyu Twite huku Mtibwa ikiwatoa Ibrahim Jeba na Chanongo na kuwaingiza Husein Javu pamoja na Kelvin Friday.
Mabadiliko hayo yaliinufaisha Yanga ambayo ilipata bao la tatu kupitia kwa Ngoma dakika ya 79 akiunganisha pasi nzuri ya Mwashiuya aliyoichonga kutoka winga ya kushoto.
Dakika ya 88, Tambwe aliumia baada ya kugongana na Shaban Nditi na kushindwa kuendelea na kusababisha timu yake icheze pungufu kwa sababu walikuwa wamemaliza nafasi za kufanya mabadiliko.
Yanga sasa wamefikisha pointi 14 wakiwa na michezo saba ya ligi hiyo huku wakiwa na mchezo mmoja wa kiporo mkononi.
Post a Comment