WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wanathibitisha kuwa msimu huu
wamesajili kikosi kipana kilichosheheni nyota kadhaa baada ya juzi kuibuka
Mohammed Ibrahim na kuwa shujaa wa timu hiyo kwenye pambano lao dhidi ya Mwadui
FC.
Ibrahim aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar kwenye mchezo huo
walioibuka na ushindi wa mabao 3-0, alionyesha kiwango cha hali ya juu na
kufunga mabao mawili huku akisaidia bao la tatu alilofunga Shiza Kichuya.
Mashabiki wengi wakiwa na mawazo ya Kichuya, Laudit Mavugo
na Fredrick Blagnon, Mo alithibitisha kikosi hicho msimu huu mtu yeyote anaweza
kufunga.
Simba ambao wana pointi 32 wakiongoza kwenye msimamo wa Ligi
Kuu Bara, ubora wa kikosi chao unawafanya kuendelea kufanya vema kwenye michezo
mbalimbali.
Awali alianza Mavugo kuzifumania nyavu na watu wote
wakahamishia macho yao kwa straika huyo wa Burundi, lakini baadaye aliibuka
Kichuya anayeongoza kwenye msimamo wa wafungaji kwa mabao manane.
Ukiacha Kichuya na Mavugo, aliibuka kiungo Muzamir Yassin
mwenye mabao manne kwa sasa huku straika wa Ivory Coast, Blagnon akiwa
amezifumania nyavu mara moja msimu huu, straika kipenzi cha mashabiki, Ibrahim
Ajib, naye amezifumania nyavu mara tatu msimu huu.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, amekuwa akionekana
kutopata shida ya kutafuta wachezaji baada ya kila mmoja kumpa nafasi ya
kucheza kwenye kikosi hicho.
Tofauti na misimu iliyopita Simba ilikuwa na uhaba wa
wachezaji ndiyo sababu iliyopelekea kikosi hicho kushindwa kutwaa ubingwa na
kuambulia nafasi ya tatu huku Yanga na Azam wakiendelea kupokezana kwenye
nafasi ya kwanza na ya pili.
Post a Comment