KUTOKANA na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi,
Laudit Mavugo ambaye anaichezea Simba kwa sasa kushindwa kuendelea kuonyesha
makali yake, amejitokeza na kuwataka mashabiki wa Simba kumpa muda, kwani anaamini
atafanya vyema.
Mavugo ambaye alisajiliwa Simba akitokea Vital’O
ya kwao Burundi, mara ya mwisho kufunga bao ilikuwa ni Oktoba 23 dhidi ya Toto
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar lakini kabla ya hapo alikuwa amecheza mechi sita
mfululizo bila kufunga bao lolote.
Juzi Jumamosi kwenye mchezo dhidi ya Mwadui mjini
hapa alishindwa tena kucheka na nyavu. Alipata nafasi kibao lakini alizipoteza
kabla ya kocha Joseph Omog kumtoa katika dakika ya 42 kipindi cha kwanza.
Baada ya mchezo huo, Mavugo ambaye alianza ligi
kwa mbwembwe na kuonekana atakuwa supastaa wa Simba, alisema: “Kiukweli naomba
mashabiki wa Simba wanipe muda kwani bado sijazoea baadhi ya viwanja vya hapa
Tanzania, kwani kuna viwanja vizuri lakini pia vingine ni vibovu.
“Kule kwetu Burundi hakuna viwanja vibovu kama
huku Tanzania, ndiyo maana kule nilikuwa nafunga mabao mengi lakini huku napata
tabu sana jinsi ya kufunga lakini nina imani kuwa nitayazoea mazingira na
nitafanya vema.”
Juzi, Mavugo ambaye msimu huu tayari ana mabao
manne, alikosa mabao matatu ya wazi na kulazimika kutolewa nje mapema kabisa na
nafasi yake ikachukuliwa na Ame Ally aliyeiimarisha safu ya ushambuliaji ya
Simba huku akitoa pasi ya bao la tatu la klabu hiyo lililofungwa na Mohammed
Ibrahim.
Post a Comment